• HABARI MPYA

    Tuesday, February 28, 2012

    MARIGA ACHAFUA HALI YA HEWA KENYA



    KIUNGO wa kimataifa wa Kenya, Macdonald Mariga, ataikosa mechi ya timu yake, Harambee Stars dhidi ya Togo leo, kutokana na kile kilichoelzwa kutofautiana na kocha Francis Kimanzi.
    Habari za ndani zinasema kwamba, Mariga alitarajiwa kusafiri kurejea katika klabu yake ya Italia, Parma jana usiku na ameamua kutocheza tena timu ya taifa chini ya kocha Francis Kimanzi.
    Lakini suala hilo linalozungumziwa juu ya kuondoka kwake ni gharama za tiketi zake kuja nchini, ingawa ukweli ni kwamba ana ‘bifu’ na Kimanzi.
    "Mariga hana furaha na atasafiri leo (jana) kurejea Italia ambako anatarajiwa kucheza mechi za mwishoni mwa wiki. Anafikiri kocha Kimanzi hamheshimu na hamtaki kwenye timu, kwa sababu kuna wakati aliumizwa na maneno ya kocha huyo aliposema kama akitakiwa kuchagua mchezaji mmoja kati yake na Oliech, atampiga chini Mariga," kilisema chanzo.
    Alipotakiwa kuzungumzia habari hizo, Kimanzi kwanza alicheka sana: "Vipi wanaweza kusema simtaki Mariga na tayari nimemuita kwenye timu katika kila mchezo tangu nimeanza kazi. Waache kupika majungu na kutatua matatizo yanayowakabili, kuliko kutafuta sababu," alisema Kimanzi.
    Mariga aligoma kucheza juzi hadi arejeshewe fedha za tiketi alizokopwa, lakini hilo ni jukumu la shirikisho la soka Kenya, kwake na wachezaji wengine waliotumia tiketi zao kurejea nyumbani kurejeshewa fedha zao.
    Lakini upande wa pili, Mariga anaonekana mkorofi na asiye na nidhamu wala uzalendo.
    “Mariga angeacha kusumbua na madai yake. Ni kwa bahati mbaya kwamba hata Nahodha Dennis Oliech hajalipwa baadhi ya fedha zake alizotumia kwa tiketi ya ndege, lakini hatujamuona kupiga kelele kwamba hatacheza.
    "Watu kama Jamal Mohamed pia wamekopwa na uongozi uliopita wa shirikisho na hata Victor Mugubi aliongeza fedha na kukata tiketi ya daraja la kwanza, lakini kwa Mariga wakati wote ananunua daraja la kwanza na anataka arejeshewe," alisema kiongozi mmoja wa juu wa KFF.
    Mariga aliichezea mara ya mwisho Harambee Stars Oktoba mwaka jana dhidi ya Uganda katika sare ya bila kufungana na Uganda mjini Kampala, lakini alikosa mchezo wa kuwania tiketi ya Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Shelisheli kutokana na kuwa majeruhi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MARIGA ACHAFUA HALI YA HEWA KENYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top