• HABARI MPYA

    Saturday, February 25, 2012

    MSUMBIJI WATUA KESHO TAYARI KWA MTANANGE JUMATANO

    WAKATI maandalizi ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars dhidi ya Msumbiji, Mambas, mechi itakayopigwa Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika yanaendelea vizuri, wapinzani wao hao wanatarajiwa kuwasili nchini leo, tayari kwa mchezo huo. Mambas, wenye rekodi nzuri wanapocheza Dar es Salaam dhidi ya Stars, watatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ndege ya shirika la ndege la Afrika Kusini, saa 7.55 mchana.
    Msafara wa Mambas kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumatano (Februari 29 mwaka huu) saa 10 kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, utakuwa na watu 29, kati ya hao, 19 ni wachezaji wakati waliobaki ni maofisa wa timu hiyo.
    Refa wa mechi hiyo, Farouk Mohamed na wasaidizi wake, Ayman Degaish, B.T Abo El Sadat na Gihed Greisha kutoka Misri watawasili nchini leo kwa ndege ya shirika la ndege la Misri na Kamisaa Loed Mc Ian kutoka Afrika Kusini.
    Tiketi za mechi hiyo zinatarajiwa kuanza kuuzwa keshokutwa katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha Mafuta cha Bigbon kilichopo Msimbazi (Kariakoo), Mgahawa wa Steers ulioko Barabara ya Samora/Ohio, Kituo cha Mafuta cha Oilcom Ubungo na Uwanja wa Taifa.
    Kikosi cha Stars kilichopo kambini kwa ajili ya mchezo huo kinaundwa na makipa; Shaaban Kado (Yanga), Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ali (Azam), mabeki Stefano Mwasyika na Nsajigwa Shadrack (Yanga), Nassor Masoud ‘Chollo’ Juma Nyoso, Juma Jabu na Kelvin Yondani (Simba) na Aggrey Morris (Azam).
    Viungo ni Jonas Gerard, Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto (Simba), Shaaban Nditi (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar na Abdi Kassim (Azam) na washambuliaji ni Hussein Javu (Mtibwa Sugar), John Bocco, Mrisho Ngassa (Azam), Uhuru Suleiman (Simba) na Nsa Job (Villa Squad).
    Nizar Khalfan wa Philadelphia Union ya Marekani na Ally Badru Ally wa Canal Suez ya Misri bado hawajawasili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUMBIJI WATUA KESHO TAYARI KWA MTANANGE JUMATANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top