• HABARI MPYA

    Tuesday, October 15, 2019

    YANGA SC INA UWEZO WA KUIFUNGA PYRAMIDS CCM KIRUMBA WIKI IJAYO

    Na Dominick Salamba, DAR ES SALAAM
    KATIKA msimu huu wa 2019/2020  ni miongoni mwa misimu ambayo itakumbukwa sana kwani tumeshuhudia Tanzania bara ikipata nafasi ya kutoa timu 4 katika michuano ya Kimataifa Barani Afrika,kwa maana timu mbili za Yanga SC na Simba SC katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika huku Azam FC na KMC  wakiwa wawakilishi wa michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika.
    Lakini katika hali isiyo ya kuvutia mpaka sasa wawakilishi watatu kwa maana ya Simba SC,Azam FC na KMC tayari wameyaaga mashindano hayo katika hatua za mwanzo huku timu pekee iliyobaki ni Yanga SC huku wakiwa sio sehemu ya michuano ya Klabu Bingwa badala yake wanawania nafasi ya kuingia makundi katika kombe la Shirikisho..
    Yawezekana kuna sababu nyingi zimepelekea kupoteza timu tatu katika hatua hizi mbili lakini yote kwa yote bado sijaona malengo ya juu katika kuwa washiriki wa kweli kwenye michuano hii,kwani hutakiwi kushiriki kwakuwa nafasi imepatikana bali inatakiwa ushiriki ukiwa na malengo,nia na mipango ili kuona unakuwa na ushindani katika michuano hii mikubwa kabisa Barani Afrika.
    Turudi kwa wawakilishi waliobaki ambao ni Yanga SC na wataanzia mchezo wao katika dimba la Kirumba jijini Mwanza siku ya jumapili ya Tarehe 27/10/2019 kwa kuumana na timu inayokuja kwa kasi katika  ushindani wa soka la Afrika Pyramid FC kutoka nchini Misri.
    Pyramid FC ni timu changa ukilinganisha na Yanga SC kwa maana ya historia yake na hata uzoefu wa kushiriki katika michuano hii mikubwa na haijawahi kuchukuwa ubingwa wowote iwe nchini Misri au katika michuano ya Afrika kwani ndio msimu wake wa kwanza kushiriki ikiwa imeanzishwa mwaka 2008 na kupanda ligi kuu nchini mwao mwaka 2014 huku msimu uliopita ikimaliza katika nafasi ya  3 na kupata nafasi ya kushiriki michuano hii ya pili kwa ukubwa barani Afrika kwa upande wa vilabu.
    Ni timu ambayo inapatikana katika jiji la Cairo ambayo uwanja wake wa nyumbani unaitwa 30 June Stadium   wenye uwezo wa kubeba watu elfu 30.
    Katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikijipenyeza katika kutafuta ufalme katika soka la Misri kwa kupata matokeo katika mechi dhidi ya vilabu vikubwa vya nchini mwao kama Al Ahly na Zamalek jambo lilopelekea kuwa miongoni mwa timu zinazozungumzika sana nchini mwao hasa kutokana na uwekezaji mkubwa waliofanya kwa kusajili wachezaji wa gharama na wenye uwezo mkubwa kutoka mataifa mbalimbali ambayo yamepiga hatua kisoka,wachezaji kama Wilfred Kanon mwenye miaka 26 Mlinzi wa kati kutoka Ivory Coast,Erick Traore mwenye miaka 23  winga wa kulia kutoka  Burkinafaso,John  Antwi mwenye miaka 27 mshambuliaji kutoka Ghana na Lumala Abdu mwenye miaka 22 mshambuliaji kutoka Uganda.
    Aina ya uchezaji wake ni tofauti na timu nyingine kutoka Afrika kaskazini ambazo zinapocheza ugenini uja kwa kujilinda zaida hawa Pyramid FC wanacheza tofauti wao ushambulia na kutafuta ushindi nyumbani na ugenini hivyo namna ya kuwakabili inakuwa tofauti ukilinganisha na timu nyingine kutoka ukanda huo.
    Nimeanza kwa kueleza machache ili Yanga SC waijue japo kwa uchache na nadhani na wao watakuwa wamesha wachunguza vya kutosha na kujua ubora na udhaifu wa wapinzani wao ambao wameamua kuwapeleka Mwanza katika mechi yao ya Tarehe 27 mwezi huu.
    Bado naona Yanga SC wanaweza kupata matokeo endapo watarekebisha makosa ambayo wamekuwa wakiyafanya hasa katika michuano hii kwani silaha kubwa ya kupata mafanikio katika michuano mikubwa Barani Afrika kwa vilabu au Timu ya Taifa ni kutumia vema uwanja wa nyumbani jambo ambalo Yanga SC linawasumbua sana sana,wamekuwa na wakati mgumu sana katika mechi za nyumbani tofauti wanapokuwa ugenini sio tu kimatokeo ila hata uchezaji wakiwa ugenini wanacheza vizuri zaidi hata kama wanapoteza tofauti na wanapokuwa nyumbani,jambo ambalo linaonekana kuwaingia hata wachezaji na kuamini kuwa wanaweza fanya vema ugenini kuliko nyumbani lakini kipindi hiki wanakutana na timu kutoka kaskazini mwa Afrika ambao shughuli inafahamika wakiwa kwao.
    Hivyo kwa kuanzia Yanga SC wanatakiwa kurekebisha hilo la matumizi ya uwanja wa nyumbani ili kuwa na mtaji mzuri katika mchezo wa marudiano.
    Pia ni vema benchi la ufundi kuiandaa timu kwa kucheza mchezo wa kushambulia tena ni vema kama mechi ikianza mapema huku wakitumia winga na mipira mirefu jambo ambalo litawachosha wapinzani na kuwamaliza mapema katika jiji la Mwanza.
    Timu inatakiwa kuwahi mwanza na kuzoea hali ya hewa na hali ya kiwanja kwani wasije wakajikuta nao wanakuwa wageni mwenyeji kwani hali ya Mwanza si sawa na Dar -es-salaam lakini pia uwanja wa kirumba haupo sawa na uwanja wa Taifa ambao umekuwa ukitumiwa na Yanga SC katika michezo yake mikubwa kwa hiyo kuna haja ya kuwahi ili waweze kutumia vizuri maamuzi yao ya kupeleka mechi Mwanza.
    Mashabiki wa Yanga SC wote ni wakati wa kuungana na kuisapoti timu kwani kama inavyosemwa kuwa ni Timu ya wananchi kwa maana ni ya Watanzania na uongozi umelithibitisha hilo kwa kuwapa nafasi wananchi wa kanda ya ziwa kuishuhudia timu yao katika dimba la kirumba hivyo ni wakati wa wao kuonesha kuwa uongozi haukukosea na pengine kuendelea kuwafanya viongozi waamue kuendelea kuifanya timu icheze mwanza,hivyo jukumu lao ni kuujaza uwanja,kutoa hamasa ya kutosha kwa timu kipindi chote ambacho timu itakuwa uko na kufanya Yanga itinge makundi ikitokea mwanza ni nafasi adhimu ambayo wanayanga wengine katika kanda zingine nao wangetamani kuipata hivyo ni vema wakatumia fursa hiyo wana yanga wa kanda ya ziwa..
    Wadau wote wa soka Tanzania tuwajibika kuwaunga mkono Wana Yanga sc kwani ndio wawakilishi pekee waliobaki katika michuano ya Afrika lakini tukumbuke kuwa uwakilishi wa timu 4 unatokana na kufanya vizuri katika michuano hii  sasa tumebaki na timu moja na tunahitaji kuendelea kuwa na timu 4 hivyo ni vema kuhakikisha Yanga SC wanaingia makundi na kutuongezea alama za kutufanya tubakie na wawakilishi 4 hivyo kwa maslahi mapana ya soka letu tuungane na kuwa kitu kimoja.
    Mwisho niwatakie maandalizi mema kikosi cha Yanga SC kwani watambue kuwa Taifa lipo nyuma yao katika hili  hivyo wanapaswa kujitoa hasa kuhakikisha wanaipeperusha vema bendera ya nchi yetu..
    MUNGU ibariki Yanga SC. MUNGU ibariki Tanzania

    (Dominick Salamba ni mchambuzi wa soka anapatikana pia kupitia katika Akaunti zake za mitandao ya kijamii kupitia: Instagram: @dominicksalamba Facebook: dominicksalamba Twitter: dominicksalamba, au namba ya simu +255 713 942 770)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC INA UWEZO WA KUIFUNGA PYRAMIDS CCM KIRUMBA WIKI IJAYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top