• HABARI MPYA

    Thursday, October 24, 2019

    VAR YAKATAA BAO LA SAMATTA KRC GENK YACHAPWA 4-1 NA LIVERPOOL LIGI YA MABINGWA ULAYA

    Na Mwandishi Wetu, GENK 
    REFA Mslovenia, Slavko Vincic jana alikataa kwa la mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta, timu yake, KRC Genk ikifungwa 4-1 na mabingwa watetezi, Liverpool katika mchezo wa Kundi E Ligi ya Mabingwa Ulaya Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
    Refa huyo alikataa bao hilo lililofungwa na Nahodha huyo wa KRC Genk dakika ya 26 kwa kichwa akiunganisha krosi ya Junya Ito, baada ya kurudia kutazama picha za video na kujiridhisha Mtanzania huyo alikuwa ameotea wakati anafunga.
    Bao hilo lingekuwa la kusawazisha baada ya Liverpool inayofundishwa na kocha Mjerumani, Jurgen Klopp kutangulia kwa bao la nyota wa England, Alex Oxlade-Chamberlain dakika ya pili, ambaye alifunga la pili pia dakika ya 57. 
    Mbwana Samatta akimlalamikia refa Mslovenia, Slavko Vincic jana baada ya kukataa bao lake
    Mbwana Samatta alifunga katikati ya mabeki wawili wa Liverpool, lakini bado haikusaidia

    Mabao mengine yote yalifungwa na washambuliaji wa Kiafrika, Sadio Mane kutoka Senegal dakika ya 77 na Mohamed Salah wa Misri dakika ya 87 upande wa a Liverpool, huku la Genk likifungwa Mnigeria Stephen Odey dakika ya 88.
    Genk inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Felice Mazzu inabaki na pointi yake moja baada ya mechi tatu, ikifungwa mbili na kutoa sare moja, ikiendelea kushika mkia, wakati Liverpool inayofikisha pointi sita baada ya kushinda mechi moja na kufungwa moja kati ya mbili za mwanzo sasa ni ya pili Kundi E.
    Napoli ya Italia sasa ndiyo inaongoza kundi hilo baada ya ushindi wa 3-2 dhidi ya wenyeji, Salzburg jana jan na kufikisha pointi saba. Salzburg inabaki na ponti zake tatu katika nafasi ya tatu. 
    Samatta jana amecheza mechi ya tatu tu Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa amefunga bao moja katika mchezo wa kwanza KRC Genk wakichapwa 6-2 na Salzburg nchini Austria.
    Kwa ujumla Samatta jana amecheza ya 169 kwenye mashindano yote tangu ajiunge na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa amefunga mabao 68.
    Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 132 na kufunga mabao 52, kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, katika Super Cup mechi moja na Europa League mechi 24 na mabao 14.
    Kikosi cha KRC Genk jana kilikuwa; Coucke, Maehle, Cuesta, Lucumi, Uronen, Ito, Heynen, Berge, Bongonda/Ndongalaat 66, Samatta na Onuachu/Odey dk81.
    Liverpool; Alisson, Milner, Lovren, Van Dijk, Robertson/Gomez dk63, Oxlade-Chamberlain/Wijnaldum dk74, Fabinho, Keita, Salah, Firmino/Origi dk80 na Mane.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VAR YAKATAA BAO LA SAMATTA KRC GENK YACHAPWA 4-1 NA LIVERPOOL LIGI YA MABINGWA ULAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top