• HABARI MPYA

  Monday, August 05, 2019

  WAZIRI DK. MWAKYEMBE AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA UWANJA WA SIMBA SC BUNJU

  Na Asha Said, DAR ES SALAAM
  WAZIRI wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe asubuhi ya leo ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Uwanja wa klabu hiyo eneo la Bunju mjini Dar es Salaam.
  Akiwa ameongozana na Mwenyekiti wa Bodi ya Ukurugenzi ya klabu ya Simba SC, Mohammed ‘Mo’ Dewji, Waziri Mwakyembe aliweka jiwe hilo katika eneo hilo ambalo tayari zoezi la ujenzi limeanza.
  Akizungumza kwenye hafla hiyo, Dewji alisema kwamba akiwa mwanachama na mpenzi wa Simba SC ameamua kutoa fedha zake kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa Uwanja huo.

  Waziri Dk. Harrison Mwakyembe (kulia) akimsikiliza Mohammed 'Mo' Dewji (kushoto)

  Dewji akasema kwamba wataandaa usiku maalum ‘Gala’ wa kuwaalika wapenzi na wanachama wa Simba SC wapatao 500 kwa ajili ya kuchangia fedha maalum kwa awamu ya pili ya ujenzi, ambao kwa ujumla itahusu viwanja vya nyasi asilia na nyasi bandia, vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji na uzio wa eneo lote.
  “Naomba nitoe ufafanuzi, fedha hizi nilizotoa hazihusiani na zile tulizokubaliana kuwekeza ndani ya Simba SC,”alifafanua Dewji aliyeshinda zabuni ya uwekezaji kwenye klabu hiyo kwa dau la Sh. Bilioni 20.
  Dewji amesema kwamba dhamira yake ya kuona Simba siyo tu inashinda kila taji inalowania , lakini pia iwe na miundombinu bora na ya kisasa itakayaoiwezesha kuzalisha na wachezaji vijana watakaotokana na mipango ya muda mrefu na mfupi, kuhakikisha inakuwa na kikosi bora zaidi ya ilichonacho sasa.
  “Baada ya miaka kadhaa ya kutokuwa na uwanja wetu rasmi, leo klabu hii kubwa kabisa nchini hatimaye tunatimiza ndoto zetu. Nimefanya haya kutokana na mahaba yangu makubwa kwa klabu hii ninayoishabikia toka utoto,”.
  Mo Dewji pia amesema anataka kununua timu ya daraja la kwanza aibadilishe jina iitwe Simba B, ili ishiriki ligi hiyo, lakini ikipanda haicheza Ligi Kuu kwa sababu hawataruhusiwa kuwa na timu mbili za ligi hiyo kubwa nchini.
  Mabingwa hao wa Tanzania kesho jioni watamenyana na Power Dynamos ya Zambia Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika mchezo wa kirafiki kuazimisha kilele cha Wiki ya Simba, maarufu kama Simba Day.
  Ni siku ambayo rasmi klabu itazinduia jezi zake za msimu mpya na kutambulisha kikosi kipya kuelekea msimu huo utakaofunguliwa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Simba SC wataanzia ugenini dhidi ya UD do Songo ya Msumbiji kati ya Agosti 9 na 11 kabla ya kurejea nyumbani kwa mchezo wa marudiano kati ya Agosti 23 na 25.
  Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza, Simba itakutana na mshindi kati ya FC Platinum ya Zimbabwe na Nyasa Bullets ya Malawi na ikifuzu mtihani huo pia itaingia tena hatua ya makundi.
  Ikumbukwe Simba ilirejea Dar es Salaam wiki iliyopita baada ya kambi ya zaidi ya wiki tatu mjini Rusternburg, Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya.
  Na ikiwa huko ilipata mechi nne za kujipima nguvu, ikishinda mbili na kutoa sare mbili. Ilishinda 4-1 dhidi ya Orbit Tvet, 4-0 dhidi ya Platinums Stars kabla ya sare mbili mfululizo za 1-1 dhidi ya Township Rollers ya Botswana na Orlando Pirates ya Johannesburg.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAZIRI DK. MWAKYEMBE AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA UWANJA WA SIMBA SC BUNJU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top