• HABARI MPYA

  Monday, August 05, 2019

  TAIFA STARS WAREJEA DAR KISHUJAA BAADA YA KUING’OA KENYA MBIO ZA CHAN MWAKANI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kimerejea leo Dar es Salaam kishujaa badaa ya kutinga hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya Fainali za Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) mwakani nchini Cameroon..
  Hiyo ni baada ya ushindi wa penalti 4-1 dhidi ya Kenya jana jioni Uwanja wa Moi Kasarani mjini Nairobi, Kenya, kipa mkongwe Juma Kaseja akiibuka shujaa baada ya kupangua penalti ya Michael Kibwage kufuatia kurejeshwa kikosini baada ya miaka sita.
  Waliofunga penalti za Tanzania ni mabeki Erasto Nyoni, Paul Godfrey ‘Boxer’, Gardiel Michael na mshambuliaji Salum Aiyeee.

  Rais wa TFF, Wallace Karia (aliyesimama) akiwa na wachezaji wa Taifa Stars

  Kenya walipata penalti moja tu, ambayo ilifungwa na Cliffton Miheso Ayisi, huku nyingine wakikosa Michael Kibwage na Joash Achieng Onyango.
  Sasa Tanzania itakutana na Sudan katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya CHAN ya mwakani nchini Cameroon, mechi ya kwanza ikichezwa Dar es Salaam Septemba 20 na marudiano Oktoba 18 Khartoum.
  Makocha Mrundi, Ettienne Ndayiragijje wa Azam FC na Wasaidizi wake, Juma Mgunda wa Coastal Union ya Tanga na Suleiman Matola wa Polisi Tanzania wanarejea kwenye klabu zao kwa maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu kwa sasa sawa na wachezaji.
  Baadaye Ndayiragijje anatarajiwa kuwa na kikao na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwasilisha ripoti ya hatua iliyopita na programu ya maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Sudan.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAIFA STARS WAREJEA DAR KISHUJAA BAADA YA KUING’OA KENYA MBIO ZA CHAN MWAKANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top