• HABARI MPYA

  Thursday, August 02, 2018

  SAMATTA: NAPENDA KUCHEZA HISPANIA NA ENGLAND, LAKINI SITAKI KUONDOKA VIBAYA GENK

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WIKI iliyopita ziliibuka habari za Nahodha wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta kutakiwa na klabu mbalimbali za Ulaya, zikiwemo Levante ya Hispania, Leicester City, West Ham Unted za England, Borussia Dortmund ya Ujerumani na CSKA Moscow ya Urusi.
  Na kufuatia taarifa hizo, Bin Zubeiry Sports – Online ikafanya mahojiano kwa simu kutoka Ubelgiji jana na Samatta aliyejiunga na Genk  Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili kufahamu zaidi kutoka kwake yeye mwenyewe. Endelea.
  Mbwana Samatta (kushoto) anasema Taifa Stars ina nafasi ya kufuzu AFCON  

  Bin Zubeiry Sports – Online; Habari za leo Nahodha
  Mbwana Samatta; Nzuri, vipi wewe
  Bin Zubeiry Sports – Online; Salama namshukuru Mungu, utakuwa tayari kwa mahojiano kidogo? 
  Mbwana Samatta; Bila shaka, karibu
  Bin Zubeiry Sports – Online; Kumekuwa na mfululuzo wa habari za kutakiwa na timu za Hispania, England na Ujerumani. Una taarifa zozote rasmi?
  Mbwana Samatta; Ningependa kwa sasa nisilizungumzie hilo hadi muda ukiwa tayari
  Bin Zubeiry Sports – Online; Sawa. Na vipi msimu mpya kwako umeanzaje?
  Mbwana Samatta; Nimeanza vizuri kabisa na ninaamini na nina nia ya kufanya msimu wangu uwe bora sana
  Bin Zubeiry Sports – Online; Kikosi cha Genk msimu huu kina mabadiliko yoyote hadi sasa?
  Mbwana Samatta; Ni sahihi kuna wachezaji wapatao watano wapya katika nafasi tofauti tofauti
  Bin Zubeiry Sports – Online; Na wote wameingia kikosi cha kwanza au?
  Mbwana Samatta; Hapana bado hawajaingia wote, wa kikosi cha kwanza ni waliokuwepo msimu uliopita
  Bin Zubeiry Sports – Online; Unadhani ni wakati mwafaka kuondoka Ubelgiji kwa sasa?
  Mbwana Samatta; Nafurahi kutimiza ndoto zangu, tangu nikiwa mdogo nilikuwa nikitamani kucheza soka Ulaya na kwa sasa nipo Ulaya nacheza soka. Sipendi kujipa presha kubwa katika maisha yangu, napenda kucheza Ligi za England, au Hispania, lakini nahitaji kuweka mizizi imara hapa ili nipate njia ya kuwapenyeza wengine kutoka Tanzania. Kwa hiyo sipendi kuwe na aina yoyote ya maelewano mabaya isipohitajika.
  Bin Zubeiry Sports – Online; Na Genk wanakupa heshima ya kukuridhisha?
  Mbwana Samatta; Mahusiano ya kuridhisha na kila mmoja klabuni
  Bin Zubeiry Sports – Online; Kutoka TP Mazembe hadi Genk, baada ya miaka mitatu kwako binafsi umeona mabadiliko gani ya ndani na nje ya Uwanja?
  Mbwana Samatta; Mabadiliko kiasi fulani yapo, lakini kubwa ni jinsi ambavyo naelewa zaidi kwa upana mchezo wa mpira wa miguu na nini kama mchezaji natakiwa nifanye ili kuwa katika kiwango bora.
  Bin Zubeiry Sports – Online; Wachezaji wengi wa Kiafrika wanapomaliza mpira huhamishia maisha yao Ulaya, baada ya miaka mitatu ya kuwa huko unafikiria nini kwa upande wako
  Mbwana Samatta; Sehemu ambayo naijua zaidi ni hapa Ubelgiji, inawezekana naweza kuwa na wazo jipya nikipata nafasi kwenda sehemu nyingine. Lakini hadi sasa sijafikiria kuishi huku, nadhani sehemu ya pili inayonivutia ukiondoa Tanzania basi ni Afrika Kusini.
  Bin Zubeiry Sports – Online; Kwa mafanikio yako wewe ni mchezaji mkubwa sana kihistoria katika soka ya Tanzania, unafikiria kufanya nini zaidi kwa nchi yako kwa heshima na kumbukumbu ya kudumu?
  Mbwana Samatta; Napenda kuanzisha kituo cha kulea na kukuza wachezaji na pia kuwa na kampuni ya kumiliki wachezaji yenye nguvu na ushirikiano na klabu za Ulaya ili iwe rahisi kwa watoto wengi wa Kitanzania kutimiza ndoto zao kama ilivyotokea kwangu.
  Bin Zubeiry Sports – Online; Umekwishafanya chochote hadi sasa katika kutekeleza hayo?
  Mbwana Samatta; Nisingependa kuliweka wazi kwa sasa
  Bin Zubeiry Sports – Online; Ubelgiji wamerejea na Medali za Shaba kutoka Urusi, bila shaka ni furaha kubwa sana huko
  Mbwana Samatta; Ni sahihi, kufika Nusu Fainali katika mashindano makubwa kama Kombe la Dunia siyo jambo rahisi.
  Bin Zubeiry Sports – Online; Vipi wewe na timu yako ya taifa. Hali ikoje?
  Mbwana Samatta; Unakosea kusema timu yangu, bali ni timu ya Watanzania wote.
  Bin Zubeiry Sports – Online; Ok wewe na timu yenu ya taifa hali ikoje?
  Mbwana Samatta; Baada ya muda mrefu sasa tunapata wachezaji wengi wanaocheza nje, nina imani wataibadilisha timu ya taifa, muda mfupi ujao tutaanza kufurahia ubora wa timu ya taifa.
  Bin Zubeiry Sports – Online; Kuelekea mechi na Uganda Septemba 8, nini wito wako kwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania)
  Mbwana Samatta; Wanajua wanachokifanya, wako makini sina wito kwao.
  Bin Zubeiry Sports – Online; Kama Nahodha, huwa unashirikishwa na TFF katika mambo muhimu kuhusu timu ikiwemo masuala ya uteuzi wa makocha na wachezaji?
  Mbwana Samatta; Nisingependa kulizungumza hilo
  Bin Zubeiry Sports – Online; Na nafasi yenu ikoje katika mbio za AFCON ya mwakani Cameroon?
  Mbwana Samatta; Mchezo wa kwanza tumeuanza kwa droo nyumbani, nadhan siyo jambo zuri sana, ila bado ninaamini nafasi ya kufuzu ni kubwa kuliko miaka iliyopita.
  Bin Zubeiry Sports – Online; Kuna malalamiko Usimba na Uyanga unaingilia hadi Taifa Stars na kuharibu mambo. Umeliona hilo?
  Mbwana Samatta; Wachezaj ndani ya timu ya taifa ni kitu kimoja, hakuna mgawanyiko.
  Bin Zubeiry Sports – Online; Nilisema mahojiano kidogo, naona ninaanza kunogewa. Niseme inatosha kwa leo Nahodha na ahsante sana kwa mara nyingine. 
  Mbwana Samatta; Hakuna shaka, ninashukuru. Nikutakie kazi njema.
  Bin Zubeiry Sports – Online; Asante, nawe pia 
  Mbwana Samatta; Asante.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA: NAPENDA KUCHEZA HISPANIA NA ENGLAND, LAKINI SITAKI KUONDOKA VIBAYA GENK Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top