• HABARI MPYA

  Thursday, March 01, 2018

  OKWI NA BOCCO WOTE HATIHATI KUICHEZEA SIMBA SC DHIDI YA STAND UNITED KESHO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Mganda wa Simba, Emmanuel Okwi jioni ya leo anatarajiwa kufanya mazoezi baada ya mapumziko ya siku tatu kufuatia maumivu ya kifundo cha mguu.
  Okwi aliumia Jumatatu wiki hii katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC kufuatia kugongana na mchezaji wa zamani wa Simba B, Boniphace Maganga na kushindwa kuendelea na mchezo baada ya dakika 80, nafasi yake ikichukuliwa na Mrundi, Laudit Mavugo.
  Okwi aliondoka uwanjani akiwa amekwishaifungia Simba mabao mawili, mengine yakifungwa na Shiza Kichuya, Erasto Nyoni na Mghana, Nicholaus Gyan.
  Pamoja na Okwi, mshambuliaji mwingine tegemeo wa timu hiyo na Nahodha, John Raphael naye anatarajiwa kuendelea na mazoezi leo baada ya kuanza jana kufuatia mapumziko ya takriban wiki mbili.
  Emmanuel Okwi (kushoto) akitolewa kwa msaada wa Daktari wa Simba, Dk. Yassin Gembe Jumatatu   
  Hapa ndipo Emmanuel Okwi alipoumia baada ya kugongana na Boniphace Maganga  
  Lakini Emmanuel Okwi aliondoka uwanjani akiwa amekwishaifungia Simba mabao mawili 

  Bocco aliumia Februari 15 katika sare ya 2-2 na wenyeji, Mwadui FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na tangu hapo amekosa mechi mbili, marudiano Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gendarmerie Tnare nchini Djibouti, Simba ikishinda 1-0 bao pekee la Okwi na dhidi ya Mbao FC. 
  Bado uwezekano wa wawili hao kucheza mechi ya kesho ya Ligi Kuu dhidi ya Stand United ni mdogo, kwani pamoja na kwamba Bocco alianza mazoezi jana, lakini anaonekana bado hajawa sawa.
  Na kama Simba itawakosa wawili hao kesho, wazi kocha Mfaransa Pierre Lechantre, anayesaidiwa na Mrundi, Masoud Juma, Mtunisia, Mohammed Aymen Hbibi na mzalendo, Muharami Mohammed ‘Shilton’, atakuwa na mtihani mgumu, kwani Bocco na Okwi ndio wamekuwa wakiibeba Simba hivi karibuni. 
  Simba SC inaendelea na mazoezi Uwanja wa Boko Veterani ikiwa imeweka kambi katika hoteli ya Sea Scape, Kunduchi, Dar es Salaam.
  Simba SC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 45 baada ya kucheza mechi 19, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 40 za mechi 19.
  Baada ya mchezo wa kesho, Wekundu hao wa Msimbazi watarejea kambini kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya El Masry ya Misri, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OKWI NA BOCCO WOTE HATIHATI KUICHEZEA SIMBA SC DHIDI YA STAND UNITED KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top