• HABARI MPYA

  Thursday, February 15, 2018

  SIMBA SC YAPUNGUZWA KASI SHINYANGA, SARE 2-2 NA MWADUI KAMBARAGE

  Na Alex Sanga, SHINYANGA
  TIMU ya Simba SC imepunguzwa kasi baada ya sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji, Mwadui FC Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga jioni ya leo.
  Sare hiyo inaiongezea pointi moja Simba SC ikifikisha 42 baada ya kucheza mechi 18, pointi tano zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC walio nafasi ya pili kwa pointi zao 37, wakifuatiwa na Azam FC yenye pointi 34.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Shomary Lawi wa Kigoma aliyesaidiwa na Janet Balama nan a Michael Mkongwa wa Iringa, Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Nahodha wake, John Raphael Bocco.
  Bocco alifunga kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na winga Shiza Kichuya kutoka upande wa kulia, baada ya Iddi Mobbu kumchezea rafu yeye mwenyewe nje kidogo ya boksi.
  Simba SC ikapata pigo dakika ya 29 baada ya mfungaji wake wa bao la kwanza, Bocco kushindwa kuendelea na mchezo kufuatia kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo.
  Pengo la Bocco lilionekana wazi, kwani baada ya kutolewa safu ya ushambuliaji ilipooza na hapo ndipo Mwadui nao walipofunguka na kuanza kusukuma mashambulizi langoni mwa Simba mfululizo.
  Pamoja na hayo, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika Simba SC wakiwa bado wanaongoza kwa bao hilo la Bocco.
  Kipindi cha pili, Mwadui walikianza kwa kasi na haikuwa ajabu walipofanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 59 kupitia kwa beki wa zamani wa Yanga SC, David Luhende aliyefunga kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 20 baada ya kiungo Mghana, James Kotei kumuangusha Awadh Juma.
  Simba SC ikapata bao la pili kwa penalti dakika ya 68, mfungaji Mganda Emmanuel Okwi akifunga bao lake la 14 msimu huu katika Ligi Kuu baada ya yeye mwenyewe, kugongwa na beki Joram Mgeveke kwenye boksi.
  Ni penalti ambayo iliwaumiza Mwadui, kwa sababu Mgeveke alimgonga kwa bahati mbaya Okwi wakati ananyoosha mguu kuondosha mpira kwenye hatari na Mganda huyo akatokea mbele ghafla wakati naye akiuwahi mpira huo.
  Mwadui FC wakatulia na kuendelea kusaka bao la kusawazisha hatimaye wakafanikiwa kupata walichokuwa wanakitafuta dakika ya 89, baada ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Paul Nonga kufunga kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabi wa Luhende.
  Na walipata bao hilo dakika tano tu baada ya beki Mganda wa Simba, Juuko Murshid kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kumchezea rafu Nonga.  
  Kocha Mfaransa wa Simba, Pierre Lechantre akampumzisha Mrundi, Laudit Mavugo na kumuingiza beki Paul Bubaka aliyekwenda kucheza faulo iliyosababisha mpira wa adhabu uliozaa bao la kusawazisha la Mwadui. 
  Kikosi cha Mwadui FC kilikuwa; Arnold Massawe, Revocatus Richard, David Luhende, Joram Mgeveke, Iddy Mobby, Awesu Ally, Jean Claude John, Awadh Juma, Paul Nonga, Evarigestus Mjwahuki na Miraji Athumani.
  Simba SC; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Juuko Murshid, Yussuph Mlipili, Erasto Nyoni, Shiza Kichuya, Said Ndemla/Nicholasu Gyan dk64, Emmanuel Okwi, John Bocco/Laudit Mavugo dk29/Paul Bukaba dk87 na James Kotei.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAPUNGUZWA KASI SHINYANGA, SARE 2-2 NA MWADUI KAMBARAGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top