• HABARI MPYA

  Friday, February 02, 2018

  COASTAL UNION YAREJEA LIGI KUU, KMC NAYO YAPANDA, POLISI DAR YAZIDI KUPOTEA

  Na Mwandishi Wetu, MOROGORO
  TIMU za Coastal Union ya Tanga na KMC ya Kinondoni, Dar es Salaam zimefanikiwa kupanda Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu ujao baada ya kushinda mechi zao za Kundi B leo.
  Coastal Union inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Juma Mgunda imeizima Mawenzi Market Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kwa kuichapa 2-0, mabao ya Raizin Hafidh dakika ya 24 na Athuman Iddi ‘Chuji’ dakika ya 72, hivyo kurejea tena Ligi Kuu misimu miwili tangu wateremke.
  Nayo KMC ya kocha Freddy Felix Minziro imeichapa 1-0 JKT Mlale Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, bao pekee la kiungo Abdulhalim Humud ‘Gaucho’.
  Wachezaji wa Coastal Union wakimpongeza Raizin Hafidh baada ya kufunga bao la kwanza dakika ya 24 leo Uwanja wa Jamhuri

  Matokeo ya mechi nyingine za leo Polisi Tanzania imeshinda 2-1 dhidi ya wenyeji Mufindi, Mbeya Kwanza imewatandika 3-1 Polisi Dar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na kuwateremsha hadi Daraja la Pili.
  Baada ya matokeo hayo, KMC inamaliza kileleni mwa Kundi B kwa pointi zake 28, ikifuatiwa na Coastal Union pointi 26, JKT Mlale pointi 25, Polisi Tanzania pointi 24, Mbeya Kwanza pointi 22, Mufindi pointi 13, Mawenzi pointi nane na Polisi Dar pointi tano.
  Ikumbukwe, JKT Tanzania, zamani JKT Ruvu imekwishapanda kutoka Kundi A na baada ya mechi za leo itajulikana timu nyingine ya kundi hilo ya kupanda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: COASTAL UNION YAREJEA LIGI KUU, KMC NAYO YAPANDA, POLISI DAR YAZIDI KUPOTEA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top