• HABARI MPYA

    Wednesday, October 05, 2016

    TFF ‘YAJIBARAGUZA’ ETI HAIJAMFUNGIA SAANYA, INAMCHUNGUZA TU…LAKINI YAKUBALI KUFUTA KADI YA MKUDE

    Na Mwandisji Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limekerwa na kuvuja kwa taarifa ya Kamati ya Saa 72 kilichoketi jana na kuwafungia waamuzi wawili wa mechi ya watani, Simba na Yanga.
    Na katika kile kinachoonekana ‘kujibaraguza’, Kamati hiyo imetoa taarifa eti haiwajafungia Martin Saanya na Samuel Mpenzu, badala yake inawachunguza.
    Lakini taarifa za uhakika kutoka kwenye kikao cha Kamati jana usiku zilisema, Saanya na Mpenzu kila mmoja amefungiwa miaka miwili.
    Taarifa rasmi ya Kamati iliyotolewa leo imesema kwamba waamuzi hao pamoja na Ferdinand Chacha sasa wanachunguzwa kwa uchezeshaji wao, lakini Simba SC imetozwa faini ya Sh. 5,000,000  na kutakiwa kufidia gharama za uharibu waliofanya Jumamosi.  
    Mashabiki wa Simba walifanya vurugu Uwanja wa Taifa Jumamosi baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
    Tambwe alifunga bao hilo dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
    Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga. Na katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
    Kwa hali hiyo, mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani. Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
    Na Mpenzu naye anadaiwa kukataa bao safi la Simba lililofungwa na Ibrahim Hajib mapema kipindi cha kwanza akidai aliotea.
    Taarifa pia imesema Kamati hiyo imefuta adhabu ya kadi nyekundu ya Mkude, baada ya kubaini hakuwa na hatia, wakati Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Hajji Manara ametozwa faini ya Sh. 200, 000 kwa kuingia uwanjani baada ya mechi.
    Katika hatua nyingine, klabu ya Azam FC imetozwa faini ya Sh. 3,000,000 kwa kosa la kuvaa nembo ya mdhamini (Vodacom) upande mmoja badala ya pande zote mbili. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF ‘YAJIBARAGUZA’ ETI HAIJAMFUNGIA SAANYA, INAMCHUNGUZA TU…LAKINI YAKUBALI KUFUTA KADI YA MKUDE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top