• HABARI MPYA

    Wednesday, October 26, 2016

    FARID MUSSA APATA KIBALI CHA KUFANYA KAZI HISPANIA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Farid Mussa Malik leo amepata kibali rasmi cha kufanya kazi nchini Hispania - maana yake mchezaji huyo wa Azam FC sasa anakwenda kuanza maisha mapya klabu ya Deportivo Tenerife.
    Taarifa ya Azam FC leo imesema kwamba, baada ya kupatikana kwa kibali hicho, sasa Mussa anatarajiwa kuondoka nchini muda wowote kuanzia sasa kwenda kuitumikia timu hiyo ya Daraja la Kwanza.
    "Tunapenda mashabiki wa soka watambue kuwa Mussa anakwenda Tenerife kwa kwa makubaliano maalumu ya pande zote mbili ukiwa ni usajili wa mkopo na Azam FC itanufaika kupitia uhamisho wake mwingine atakaposajiliwa kwenda timu nyingine barani humo,"imesema taarifa hiyo.
    Farid Mussa amepata kibali cha kufanya kazi nchini Hispania katika klabu ya Deportivo Tenerife

    Azam imesema inaamini uwepo wake kwenye klabu hiyo utafanikisha kukuza kipaji chake zaidi pamoja na thamani yake kwa ujumla, ikizingatiwa Farid bado ni mchezaji kijana anayeendelea kujifunza.
    "Kabla ya kibali hicho kutoka, kuna taarifa mbalimbali zilizotolewa zikiihusisha Azam FC kuwa tumemzuia kijana wetu huyo kujiunga na timu hiyo, lakini inaomba ieleweke kuwa kibali kilichotolewa leo hii ndicho kilichokuwa kikikwamisha uhamisho huo na tunamshukuru Mungu kimepatikana,".
    "Tunaomba ieleweke kuwa, Azam FC haitafanya jitihada zozote za kuziba milango ya wachezaji wetu pindi watakapopata timu nje ya nchi, sisi tutakuwa wa kwanza kuwaongoza katika kufikia malengo yao makubwa ya kucheza soka la kulipwa kwenye maslahi mazuri endapo taratibu za usajili zitafuatwa,".

    Azam FC imesema inaishukuru Tenerife kwa kufanikisha uhamisho huo na inanamtakia mafanikio Mussa katika maisha yake mapya ya soka.
    "Tunaamini ataitangaza vilivyo timu yetu kimataifa na Tanzania kwa ujumla jambo ambalo litafungua milango kwa wachezaji wengine kuungana naye huko,"imesema taarifa ya Azam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FARID MUSSA APATA KIBALI CHA KUFANYA KAZI HISPANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top