• HABARI MPYA

    Friday, October 21, 2016

    MANJI: GEZA ULOLE TUNAJENGA UWANJA WA MAZOEZI, MECHI ZITAKUWA KAUNDA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Yanga, Yussuf Manji amesema kwamba bado ana matumaini ya kuijengea klabu Uwanja wa kisasa eneo la Jangwani, Dar ea Salaam. 
    Aidha, Manji amesema kwamba eneo la Geza Ulole, Kigamboni anataka kuijengea timu Uwanja wa mazoezi tu mdogo na kwamba Uwanja mkubwa na wa kisasa utakuwa Jangwani.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam kuhusu Mkutano Mkuu wa dharula Jumapili, Manji aligusia pia baadhi ya mambo mengine ya maendeleo ya klabu.

    Manji akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam

    “Kule Geza Ulole tutajenga Uwanja wa mazoezi na gym. Lakini Uwanja mkubwa na wa kisasa tutajenga hapa hapa Jangwani. Kama klabu za Ulaya, Uwanja wa mazoezi unakuwa tofauti na Uwanja wa mechi,”alisema.
    Yanga inatarajiwa kuwa na Mkutano wa dharula Jumapili wiki hii Uwanja wa Kaunda, uliopo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam na Manji amewataka wanachama kujitokeza kwa wingi kujadili mustakabali wa klabu yao. 
    Ajenda kuu ya Mkutano huo ni kupitisha Baraza la Wadhamini la klabu hiyo pamoja na kuondoa Mjumbe mmoja na kuweka mpya.
    Na hayo yanafuatia Baraza la Wadhamini kuikodisha timu kwa kampuni ya Yanga Yetu kwa miaka 10, baada ya wanachama kuafiki ombi la Mwenyekiti wao, Yussuf Manji katika Mkutano wa Agosti 6, mwaka huu.
    Pamoja na hayo, Manji amesema mzee Ibrahim Akilimali amepoteza haki ya uanachama wa klabu hiyo kwa kuwa hajalipia kadi yake kwa miezi sita iliyopita.
    “Akilimali kama anataka kuja kwenye mkutano Jumapili kwanza aende kwenye tawi lake akaomba uanachama upya,” amesema Manji.
    Mwenyekiti huyo amewakaribisha wale wote wanaopinga wazo lake la kuikodisha timu katika mkutano wa Jumapili, kwani kuishia kuzungumza kwenye vyombo vya Habari haitasaidia.
    Yanga itakuwa Uwanja wake wa mazoezi Geza Ulole, Kigamboni, Dar es Salaam

    AJENDA ZA MKUTANO WA JUMAPILI KAUNDA
    1. SALA NA UTAMBULISHO WA WAGENI WAALIKWA:
    1.1. Sala ya Wakristo ya Kubariki Kikao.
    1.2. Sala ya Waislamu ya Kubariki Kikao.
    1.3. Utambulisho wa wageni waalikwa waliohudhuria, pia wenye udhuru – Waziri wa Michezo na Sanaa; Mwenyekiti wa Baraza la Michezo (BMT), Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Dar-Es-Salaam (DRFA) na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
    2. Kufungua kikao.
    3. Kupitia dondoo za kikao kilichopita cha mkutano wa wanachama na kuidhinisha.
    4. Kuthibitisha wajumbe wa bodi ya wadhamini na kumpumzisha mjumbe mmoja na kuongeza mjumbe mwingine kwenye baraza la wadhamini. mwenyekiti kuomba ridhaa ya kumteua mjumbe mmoja bila ya kuitisha mkutano mkuu kupunguza gharama kwaklabu. 
    5. Kupitia na kujadill muhtasari ya makubaliano ya bodi ya wadhamini kulingana na maagizo ya wanachamakukodisha timu ya yanga na nembo ya yanga kwa kipindi cha miaka kumi/ na kupata maamuzi kupitia kura za wanachama. 
    6. KujadiliMmweyekiti abaki kama mwenyekiti au kulingana na maslahi yake kwenye kampuni, kama italeta mgongano katika kampuni yake inayokodisha timu ya yanga na nembo ya yanga kwa kipindi cha miaka kumi  ili kupata maamuzi kupitia kura za wanachama.
    7. Kurudia kupitia marekebisho ya katiba iliyoagizwa na wanachama kupitia vikao vyao mbalimbali na baadhi kukataliwa natff, baadhi hazijasajiliwa kazi na bmt na baadhi rita wamezikalia bila kuzifanyia kazi kwa sababu zisizojulikana. kupata msimamo wa wanachama kwa kuzingatia katiba ya yanga inayosema mikutano ya wanachama ndio yenye mamlaka ya mwisho ilimradi tu maamuzi hayo yaangukie ndani ya sheria za nchi.  na si sahihi vyombo hivyo kuingiliaa maamuzi halali ya wanachama.
    8. Kupitia utendaji wa kamati ya mashindano, ratiba ya ligi kuu bara, adhabu ya yanga kutoka wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo ambayo ilisababishwa na fujo za mashabiki wa simba.   
    9. Kupata maamuzi juu ya wanachama ambao hawafiki katika mikutano badala yake wanakuwa wasemaji wa yanga bila kuwa na mamlaka hayo na kuleta uchonganishi wa wazi ndani ya klabu, kupotsoha jamii nakuchafua majina ya viongozi wa klabu.
    10. Tarehe ya uchaguzi mdogo kujazia nafasi zilizo wazi na kupata mwongozo wakutumia katiba ipi kati ya 2010 au 2014.pamojana masahihisho baada ya 2014, au bila ya masahihisho ya 2014 yaliyoamuliwa na wanachama.
    11. Hotuba ya Mwenyekiti –maoni na msimamo wake juu ya maazimio ya wanachamakwenye kikao; kusema anayoyajua ya siri kuhusu yanga na adui wa Yanga na kufafanua wanaoleta vurugu Yanga, baadhi ni mamluki wa wafanyabiashara wenzake walioshindwa kumshinda kwa njia halali na sasa wanaitumia yanga kama sehemu pekee iliyobaki kumuumiza kupitia mbinu zinazotumika hasa kwa kuleta vurugu ndani ya yanga ili kumchafua yeye binafsi, kufanya kwao hivyo ni kushusha hadhi ya klabu na maoni yake kwa maslahi ya yanga, kipi kifanyike.
    12. Mengeniyo.
    13. Sala.
    13.1. Sala ya waislamu ya kubariki maamuzi ya mkutano. 
    13.2. Sala ya wakristo kubariki maamuzi ya mkutano.
    14. Kufunga mkutano.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANJI: GEZA ULOLE TUNAJENGA UWANJA WA MAZOEZI, MECHI ZITAKUWA KAUNDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top