• HABARI MPYA

    Monday, October 31, 2016

    YANGA WAPATA MAPOKEZI MAZURI MBEYA

    Na Mwandishi Wetu, MBEYA
    YANGA SC wamepata mapokezi mazuri mjini Mbeya baada ya kuwasili leo, kwa ajili ya mechi zao mbili mfululizo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Prisons na Mbeya City.
    Yanga waliondoka Dar es Salaam mapema asubuhi ya leo kwa ndege na kutua Mbeya baada ya saa moja, ambako walipokewa kwa tafrija na nderemo na wapenzi na mashabiki wao wa huko.
    Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara watakuwa na mechi mbili mfululizo dhidi ya Mbeya City Novemba 2 na Prisons Novemba 6, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

    Na Yanga wanawasili Mbeya siku moja tu baada ya kushinda 3-0 dhidi ya Mbao FC ya Mwanza jana Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana.  
    Ushindo huo uliotokana na mabao ya beki Mtogo, Vincent Bossou, kiungo Mkongo Mbuyu Twite na mshambuliaji Mrundi Amisi Tambwe, unaifanya Yanga ifikishe pointi 27 baada ya kucheza mechi 12 ikiendelea kushika nafasi ya pili, nyuma ya Simba SC yenye pointi 32 za mechi 12 pia. 
    Baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika timu hizo zikiwa hazijafungana, beki wa kimataifa wa Togo, Bossou akaifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 49 akimalizia kwa kichwa krosi ya Deus Kaseke, kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na Haruna Niyonzima.
    Mbuyu Twite akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 55 baada ya mpira aliorusha kuokolewa vibaya na kipa wa Mbao, Emmanuel Mgeja na kudondokea nyavuni.
    Tambwe akaifungia Yanga bao la tatu dakika ya 75 na la saba kwake msimu huu akimfuatia Shizza Ramadhani Kichuya wa Simba anayeongoza kwa mabao yake nane. Tambwe alifunga bao hilo kwa usaidizi wa Niyonzima.
    Ikumbuke Yanga iliingia kwenye mchezo huo baada ya kumrejesha kocha wake Mhoalanzi Hans van der Pluijm aliyejiuzulu wiki iliyopita baada ya kukerwa na uongozi wa klabu kuleta kocha mpya, Mzambia George Lwandamina bila kumtaarifu, akisema huko ni kumvunjia heshima.
    Kocha huyo akakataa hadi nafasi ya Ukurugenzi wa Ufundi amabyo inasemekana Yanga ilitaka kumpa baada ya kumleta Lwandamina kuwa kocha Mkuu.
    Lakini baada ya kuwaaga wachezaji siku moja kabla ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKR Ruvu timu ikishinda 4-0 Jumatano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba aliingilia kati suala hilo na kuwasuluhisha hadi wakaamua kurejeana.
    Uongozi wa Yanga ulitaka kumuondoa Pluijm na Wasaidizi wake wote, Juma Mwambusi, kocha wa makipa Juma Pondamali na Meneja Hafidh Saleh wote wazalendo na kuwaleta Mzambia Lwandamina atakayekuwa Kocha Mkuu, akisaidiwa na wazalendo Charles Boniface Mkwasa, Manyika Peter kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.  

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAPATA MAPOKEZI MAZURI MBEYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top