• HABARI MPYA

    Sunday, October 23, 2016

    BADO KUSIKIA KIFUKWE SI MWANACHAMA YANGA

    KWA mara nyingine klabu ya Yanga imeingia katika mgogoro unaohusisha hadi vyombo vya dola, jambao ambalo ni kinyume na mwongozo wa Shirikisho la Soka la KImataifa (FIFA).
    FIFA inasema wazi masuala ya soka hayatakiwi kupelekwa kwenye mahakama za dola na atakayefanya hivyo ataadhibiwa.
    Adhabu kubwa ya kosa hilo ni kufutiwa uanachama, maana yake kama mtu au watu wakipeleka mambo ya soka kwenye mahakama za dola, hao si wanafamilia ya mpira wa miguu tena. 
    Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imezuia Mkutano Mkuu wa wanachama wa Yanga uliokuwa ufanyike leo Uwanja wa Kaunda, Jangwani, Dar es Salaam.
    Na hiyo inafuatia kesi iliyofunguliwa na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kwenye mahakama hiyo, kupinga mkutano huo kufanyika.
    Agizo halali la Mahakama limeuzuia uongozi wa Yanga kufanya Mkutano huo baada ya kesi iliyofunguliwa mahakamani hapo dhidi ya Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji na Kampuni ya Yanga Yetu.
    Na Manji baadaye akazungumza na Waandishi wa Habari kutangaza kuufuta Mkutano huo hadi hapo itakapotangazwa tena.
    Ajenda kuu ya Mkutano huo ilikuwa iwe kupitisha Baraza la Wadhamini la klabu hiyo pamoja na kumuondoa Mjumbe mmoja na kuweka mpya.
    Na hayo yanafuatia Baraza la Wadhamini kuikodisha timu kwa kampuni ya Yanga Yetu kwa miaka 10, baada ya wanachama kuafiki ombi la Mwenyekiti wao, Manji katika Mkutano wa Agosti 6, mwaka huu.
    Yanga Yetu ni kampuni ya Manji ambayo imeikodi klabu kwa miaka 10, baada ya kile wanachodai wenyewe kufuata taratibu.
    Lakini ukirudi kwenye ukweli – chanzo cha matatizo haya hadi kufikia kufikishwa kwenye mahakama za dola ni kutofuatwa kwa utaratibu katika zoezi hilo.
    Manji ana wazo zuri mno kwa klabu – kuiondoa timu kwenye mamlaka ya wengi ambao hawana nguvu ya kiuchumi na kuiweka mikononi mwa mtu au watu wachache wenye nguvu ya kiuchumi.
    Wazo zuri kabisa na yeyote mwenye maono ya mbali na ya kimaendeleo hawezi kupinga mpango w Manji.
    Lakini mpango wake unakutana na upinzani kutokana na namna anavyoutekeleza kama kidikteta hivi.
    Kwa kiasi fuani naweza kusema namfahamu Manji – ni mtu ambaye mara nyingi hupotoshwa na watu anaowaamini sana.
    Na ndiyo maana amekuwa akibadilisha mara kwa mara watu muhimu wa kufanya nao kazi, kama Washauri, Wanasheria na hata Wasidizi.
    Ni rahisi sana Manji kumuamini mtu, lakini pia ni rahisi sana kwake kuachana na mtu, pale anapobaini tu hakuwa mtu mzuri kwake.
    Naona dalili za kutosha- wasaidizi wa sasa wa Manji, hususan kwenye sakata hili la kuikodisha timu watapoteza nafasi zao.
    Na watapoteza nafasi zao mara tu Manji atakapobaini wanalipeleka suala hili vibaya na kuligeuza kuwa mgogoro pasipo na sababu za msingi.
    Manji anapata wapi ujasiri wa kusema Mzee Ibrahim Akilimali si mwanachama wa Yanga – na huoni iko siku atasema hata Dk, Jabir Idrisa Katundu au Injinia Francis Mponjoli Kifukwe pia si mwanachama, kwa kuwa alianza kuwatumbua akina Inspekta Hashim Abdallah, Ayoub Nyenzi na wengineo.
    Mtu yeyote wa maendeleo atakuwa anafurahia uwepo wa Manji Yanga – lakini tu anaweza akachukizwa na njia anazofanya kuelekea kujimilikisha klabu kwa sababu si njia ambazo matajiri wenzake wengine walioingia kwenye michezo walizitumia.
    Mwanasiasa na mfanyabiashara bilionea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Moise Katumbi Chapwe amekuwa Rais na mmiliki wa TP Mazembe tangu mwaka 1997 akiwa ana umri wa miaka 38 hadi sasa miaka 51.
    Hana mgogoro na mtu na wala klabu haina mgogoro kulingana na umiliki na utawala wake mzuri – lakini kwa nini Manji anataka kuigeuza Yanga kuwa kichaka cha migogoro.
    Ni Manji wa kulaumiwa kwa sababu kinachoonekana kuwa chanzo cha matatizo Yanga ni njia anazotumia za ujanja ujanja kutaka kujimilikisha klabu. Sasa ajiulize mwenyewe anakwepa nini kufuata njia halali katika kujimilikisha klabu.
    Tazama mfanyabiashara mwenzake mwenye asili ya Kiasia kama yeye, Mohamed ‘Mo’ Dewji ametoa ofa yake ya kununua asilimia 51 ya hisa za klabu baada ya hapo amekaa pembeni kuuchia uongozi uendeshe mchakato.
    Manji anataka kutumia uelewa mdogo wa wapenzi wengi wa Yanga kujichukulia klabu atakavyo yeye – kitu ambacho kinakuwa chanzo cha mgogoro hapa. 
    Yanga ni klabu kubwa na yenye historia ambayo mtu mmoja hawezi kuja kutaka kujimilikisha kimabavu kama anavyotaka kufanya Manji. Mwenyekiti yeye, Mkodishaji yeye – ni  mgongano wa kimaslahi wa kiwango gani huu! 
    Manji anataka kuwa juu wana Yanga wote. Anataka kuwa juu ya mamlaka zote za soka nchini. Anataka hadi kuwa juu ya Serikali katika mpango wake wa kujitwalia Yanga kwa gia ya kuikodi. 
    Sioni namna gani hilo linawezekana kwa sababu kwanza hao hao viongozi wa Serikali hii wanamjua vizuri na historia yake kwenye masuala ya aina hiyo.
    Watu wanapoleta hoja za kuotetea klabu, au kupingana na mawazo yake – anawaambia si wanachama. Sasa anasema Mzee Akilimali si mwanachama. Ipo siku atawavua uanachama hadi akina Kifukwe, kwani hata Akilimali si alikuwa rafiki yake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BADO KUSIKIA KIFUKWE SI MWANACHAMA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top