• HABARI MPYA

    Friday, October 28, 2016

    YANGA YAWASUBIRI BMT MLANGONI NA BARUA YA ‘KUMPIGA STOP’ MANJI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    YANGA SC inasubiri kufikishiwa katazo la maandishi na Serikali juu ya mpango wa mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu.
    Hayo yalisemwa na Kaimu Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit jana alipozungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE kuhusu agizo la Serikali kuzuia mpango wa mabadiliko katika klabu hiyo na mahasimu pia, Simba.
    “Siwezi kusema chochote kwa sasa, kwa kuwa hatujapata taarifa yoyote ya maandishi,”alisema Katibu wa Yanga jana. 
    Serikali juzi iliwashauri wafanyabiashara wenye kutaka kujimilikisha klabu za Simba na Yanga kuanzisha timu zao kama mfanyabishara mwiwngine mkubwa nchini, Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa.
    Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji (wa pili kushoto) akiwa na baadhi ya wadau wakubwa wa klabu hiyo

    Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Mohamed Kiganja alisema juzi mjini Dar es Salaam kwamba viongozi wa Simba na Yanga wanatakiwa kusitishwa michakato yote inayoendelea ya kubadilisha umiliki wa timu kutoka kwa Wanachama kwenda katika umiliki wa hisa na ukodishwaji, hadi kutakapofanyika marekebisho ya katiba zao.
    Kiganja alisema klabu hizo zinapaswa kurekebisha katiba zao kwanza kabla ya kufanya mabadiliko hayo kwa mujibu wa Sheria ya Baraza hilo na Kanuni za Msajili namba 442 Kanuni 11 kifungu kidogo cha (1-9).
    Kiganja alisema kuwa mabadiliko hayo yanayoendelea kwenye Klabu hizo tayari yameingia dosari baada ya baadhi ya Wanachama kwenda Mahakamani kupinga michakato hiyo kitu ambacho sio kizuri na pia sio ishara nzuri endapo yataachwa yaendelee.
    "Tumesitisha michakato yote ya kubadili umiliki kutoka kwa Wanachama kwenda kwa uwekezaji kwa timu za Simba na Yanga mpaka watakapo fanya mabadiliko kwa mujibu wa Katiba za Klabu zao," alisema Kiganja.
    Aidha BMT imemtaka mdau au mwanachama yoyote anayetaka kufanya uwekezaji kwenye Klabu hizo ni vema angeanzisha timu yake kama Saidi Salum Bakhresa alivyoanzisha Azam FC ili kupunguza malalamiko kwavile timu hizo zina Wanachama wengi.
    Kiganja alisema kuwa michakato hiyo ilitakiwa ianzie kwenye matawi nchi nzima ili maamuzi yawe ya wote kwani mabadiliko yoyote ndani ya klabu hizo lazima yafuate Katiba zao.
    Simba SC inataka kumuuzia mfanyabiashara na mfadhili wake wa zamani, Mohamed ‘Mo’ Dewji asilimia 51 ya hisa, wakati Yanga inataka kuikodisha timu kwa miaka 10, mfumo unaopingwa zaidi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAWASUBIRI BMT MLANGONI NA BARUA YA ‘KUMPIGA STOP’ MANJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top