• HABARI MPYA

    Thursday, October 06, 2016

    RASMI SASA YANGA NI MALI YA MANJI KWA MIAKA 10

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BARAZA la Wadhamini wa la klabu ya Young Africans SC, maarufu kama Yanga hatimaye limeikabidhi timu kwa kampuni Yanga Yetu, inayomilikiwa na Mwenyekiti wake, Yussuf Manji ambayo itakuwa mmiliki wa klabu kwa miaka 10 ijayo.
    Habari ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE imezipata kutoka ndani ya Yanga ni kwamba tayari makubaliano yamefikiwa baina ya Baraza la Kampuni ya Yanga Yetu na leo mpango huo unatarajiwa kutangazwa rasmi. 
    Mapema Agosti 6, wanachama wa Yanga walikubali kumkodisha klabu hiyo kiongozi wao huyo mkuu kwa miaka 10 na tangu hapo taratibu zimekuwa zikiendelea kimyakimya hadi mapango umekamilika.
    Yussuf Manji (katikati)  sasa ndiye mmiliki wa klabu ya Yanga kwa miaka 10 ijayo 

    Uamuzi huo ulifikiwa katika Mkutano Mkuu wa dharula uliofanyika Agosti 6, ukumbi wa Diamond jubilee, Dar es Salaam.
    Kiongozi huyo aliomba apewe klabu kwa miaka 10 na katika kipindi hicho atakuwa anachukua asilimia 75 ya mapato ya timu, huku asilimia 25 ikibaki kwa wanachama.
    Na katika kipindi hicho cha miaka 10, timu ya soka na nembo ya klabu zote zitakuwa chini yake Manji. Aidha, Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la klabu, Francis Kifukwe alisema baada ya wanachama kuridhia mpango huo, wao wanampa pia ridhaa hiyo Manji. 
    Maamuzi haya ni mwanzo wa historia mpya ndani ya Yanga, ambayo ingawa historia inasema ilizaliwa mwaka 1935 na Simba mwaka 1936, lakini ukizama ndani utagundua kwamba, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa utani na upinzani wa jadi, baina ya miamba hiyo ya soka nchini.
    Kulikuwa kuna timu inaitwa New Youngs, ambayo mwaka 1938 ilisambaratika na baadhi ya wachezaji wake wakaenda kuunda timu iliyokuwa ikiitwa Sunderland, ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba.
    Kabla ya kutokea vurugu zilizoisambaratisha New Youngs, vijana wa Dar es Salaam walikuwa wana desturi ya kukutana viwanja vya Jangwani kufanya mazoezi na baada ya muda wakaamua kuunda timu yao, waliyoipachika jina Jangwani.
    Ndani ya kipindi kifupi tu, timu hiyo iliteka hisia za wengi, waliojitokeza kujiandikisha uanachama wa klabu hiyo. Miongoni mwa waliovutika na uanachama wa klabu hiyo ni Tarbu Mangara (sasa marehemu) na ilipofika mwaka 1926, walifanya mkutano wa kwanza katika eneo ambalo hivi kuna shule ya sekondari ya Tambaza.
    Miongoni mwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuiboresha timu hiyo, ambayo wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa Bandarini na mashabiki wake wengi walikuwa wabeba mizigo wa bandarini.
    Baada ya mkutano huo, timu hiyo ilibadilishwa jina na kuwa Navigation, iliyotokea kuwa moto wa kuotea mbali katika timu za Waafrika enzi hizo, kabla ya uhuru wa Tanganyika. Timu kama Kisutu, Kitumbini, Gerezani na Mtendeni zilikuwa hazifui dafu kwa wana Jangwani hao.
    Ikiwa inatamba kwa jina la Navigation, wanachama wa timu hiyo walikuwa wakitembea kifua mbele na kuwatambia wapinzani, kwamba wao ndiyo zaidi. Kwa sababu katika kipindi hicho, Italia ilikuwa inatamba kwenye ulimwengu wa soka, wanachama wa timu hiyo nao waliamua kuibadilisha jina timu yao na kuiita Taliana.
    Taliana ilipata mafanikio ya haraka na haikushangaza ilipopanda hadi Ligi Daraja la Pili Kanda ya Dar es Salaam, mwanzoni mwa miaka ya 1930. jina la Taliana waliamua kuachana nalo mapema, kabla ya kuingia kwenye ligi hiyo, hivyo wakaanza kujiita New Youngs.
    Lakini kila ilipokuwa ikibadilisha jina, ilikuwa ikifanya vitu pia, kwani wakiwa na jina la New Youngs, waliweza kutwaa Kombe la Kassum, lililoshirikisha timu mbalimbali za Dar es Salaam. 
    Hatimaye ukawadia mwaka mbaya kwa New Youngs, 1938 wakati baadhi ya wachezaji walipojitoa na kwenda kuanzisha Sunderland. Kwa sababu hiyo, waliobaki wakaamua kubadili jina na kuwa Young Africans, jina ambalo mashabiki wake wengi walishindwa kulitamka vizuri hivyo kujikuta wakisema Yanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RASMI SASA YANGA NI MALI YA MANJI KWA MIAKA 10 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top