• HABARI MPYA

  Thursday, October 20, 2016

  SIMBA SC: HATUTAKI KUDONDOSHA HATA POINTI MOJA, NI USHINDI KWA KWENDA MBELE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAKATI leo inamenyana na Mbao FC ya Mwanza katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC imesema haitaki hata sare, inataka kushinda mechi zote kuanzia sasa.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE mjini Dar es Salaam kwamba, japokuwa Mbao FC imepanda Ligi Kuu msimu huu, lakini hawataidharau.
  “Hatupaswi kubweteka kwa matokeo mazuri ya sasa, tunatakiwa tuendelee kufanya vizuri, tusipoteze hata pointi moja. Hatutaki hata droo, lazima tushinde kila mechi, ili tuendelee kuwaacha washindani wetu katika mbio za ubingwa (Azam na Yanga),”alisema.
  Simba SC imesema inataka kushinda mechi zote kuanzia sasa

  Hajji amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi leo Uwanja wa Uhuru kuisapoti timu yao ikimenyana na Mbao inayocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu kihistoria.
  Simba SC ambayo imeweka kambi Ndege Beach Hotel, Mbweni, Dar es Salaam, ikijifua Uwanja wa Boko Veterani, itaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar mabao 2-0 Uwanja huo huo wa Uhuru.
  Simba SC inagongoza Ligi Kuu sasa ikiwa imejikusanyia pointi 23 baada ya kucheza mechi tisa, ikifuatiwa na Stand United ya Shinyanga yenye pointi 20 za mechi 10, wakati mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 18 za mechi tisa ni ya tatu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC: HATUTAKI KUDONDOSHA HATA POINTI MOJA, NI USHINDI KWA KWENDA MBELE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top