• HABARI MPYA

    Sunday, October 02, 2016

    SERIKALI YAZUIA MAPATO YOTE YA SIMBA NA YANGA HADI IKATE FIDIA YA UHARIBIFU

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    SERIKALI imezuia mapato ya mchezo wa jana baina ya Simba na Yanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hadi hapo itakapokata gharama za uharibifu uliosababishwa na vurugu. 
    Pamoja na hayo, Serikali imezizuia Simba na Yanga kutumia Uwanja wa Taifa hadi hapo itakapoamua vinginevyo.
    Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari asubuhi ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kufanya ukaguzi wa uharibifu uliofanyika.
    Waziri Nape akizungumza na Waandishi wa Habari leo Uwanja wa Taifa
    Mashabiki wa Simba jana walifanya vurugu Uwanja wa Taifa baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
    Tambwe alifunga bao lake dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
    Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.
    Katika vurugu hizo, Saanya aLImtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
    Na mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani.
    Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
    Waziri Nape akifanya ukaguzi wa athari za vurugu za jana
    Waziri Nape akiwa ameketi kwenye eneo ambalo viti vingi viling'olewa

    Nape amesema kwamba mbali na uvunjwaji wa viti, pia mageti mawili ya kuingilia, moja la upande wa Yanga na lingine wa Simba yamevunjwa.
    “Tunazuia mapato ya mechi hadi hapo tathmini itakapofanyika na kukata gharama za uharibifu uliotokea,”.
    Lakini Nape akaweka wazi kwamba ukarabati mdogo utakapokamilika Uwanja wa Uhuru, Simba na Yanga zitaruhusiwa kuendelea kutumia.
    Awali ya hapo, Kaimu Mkurugenzi wa Michezo, Alex Nkenyenge alisema kwamba zaidi ya viti 1781 vilivunjwa jana, wakati kati ya Sh. Milioni 350 na 400 zikikusanywa katika mchezo wa jana, ambao mashabiki waliingia kwa tiketi za Elektroniki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERIKALI YAZUIA MAPATO YOTE YA SIMBA NA YANGA HADI IKATE FIDIA YA UHARIBIFU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top