• HABARI MPYA

  Friday, June 03, 2016

  WAKILI KOMBA WA TFF 'AWASUSIA' YANGA UCHAGUZI WAO KISA TUHUMA ZA MANJI

  MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wakili Aloyce Komba (pichani kushoto) amejitoa kusimamia mchakato wa uchaguzi wa Yanga uliopangwa kufanyika Juni 25, mwaka huu kwa madai hataki kuwa chanzo kupotea amani katika klabu hiyo.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Dar es Salaam, Wakili Komba ametaja sababu suta za kufikia uamuzi huo, kubwa ni kulinda taaluma na heshima yake.
  "Nimetuhumiwa kupanga kumhujumu kwa kukata jina la mgombea wa nafasi ya Uenyekiti, Yussuf Manji, tuhuma ambazo zilitolewa Juni 2 mbele ya Waandishi wa Habari. Kutokana na tuhuma hizo, Manji amesema ni moja ya sababu zilizomfanya achukue fomu za kugombea uchaguzi utakaoratibiwa na Yanga," amesema.
  "Tuhuma hizo ambazo ni kubwa kwangu binafsi na zikigusa taaluma yangu ya sheria zimetolewa wakati klabu ya Yanga inahitaji amani, utulivu na mshikamano mkubwa wa wanachama, wapenzi na washabiki wake, hivyo mimi kutokuwa chanzo chochote cha vurugu zinazoweza kutokea,".
  "Tuhuma hizo zinahusu mimi kupewa fedha za hongo au rushwa (kiasi hakijulikani) ili nishawishi wajumbe wenzangu wa kamati ya uchaguzi ya TFF kukata jina la aliyekuwa mgombea mtarajiwa, Bw. Yusuf Manji kwasababu ambazo hazijaelezwa,".
  "Napaswa kupisha uchunguzi wowote huru wa tuhuma hizo nzito kama zimeshafikishwa katika vyombo vya uchunguzi wa masuala ya rushwa ili mimi nipate fursa ya kujitetea kwa uhuru zaidi,".
  "Kwa kuzingatia ushauri wa watu mbalimbali ninaowaheshimu na kuwapendasana ndani na nje ya klabu ya Yanga hususan wanasheria wengine nguli wa masuala ya michezo kama vile Wakili Sais Hamad El-Maamry, Wakili Sam Mapande, Wakili Alex Mgongolwa na waandishi wa habari waandamizi wa michezo, nimeona nisishiriki mchakato huu kwa kusimamiwa na TFF au hata ukisimamiwa na klabu ya Yanga yenyewe,".
  "Kwa kuwa mimi ni muumini mkubwa wa utawala wa sheria na hasa masuala ya katiba na demokrasia katika vilabu na vyama vya michezo, napaswa kuanzia sasa kutoshiriki vikao vyote vinavyohusu mchakato wa klabu ya Yanga nikiwa kama Mwenyekiti au Mjumbe,".
  "Nawaomba Rais wa TFF, Bw. Jamal Malinzi na Katibu Mkuu Selestine Mwesigwa na wajumbe wenzangu wa kamati ya uchaguzi ya TFF, nimemuachia madaraka ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa klabu ya Yanga, Wakili Domina Mideli, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo," imemalizia taarifa ya Komba.
  Manji jana alichukua fomu za kutetea nafasi yake makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam na kudai kwamba kuna njama zinafanywa na baadhi ya watu ndani ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakate jina lake.
  Manji wakati anawasili makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam jana

  Manji alidai kwamba alileta mpelelezi kutoka nje ya nchi akanasa mbinu hizo chafu hadi ushahidi wa sauti.
  Akasema katika sauti hizo wanasikika baadhi ya wanachama wa Yanga wakipanga njama kwa kushirikiana na watu wa TFF na BMT ili kukata jina lake katika uchaguzi.
  Akasema na hiyo ndiyo sababu hawana imani na TFF kuendesha uchaguzi wao na akasistiza Yanga itafanya yenyewe uchaguzi wake, tu kwa kusimamiwa na TFF.
  Pamoja na hayo, Manji ambaye aliwasikilizisha Waandishi wa Habari na wanachama waliokuwapo sauti hizo, akatangaza kumfuta uanachama, mwanachama ambaye sauti yake imevuma zaidi kwenye rekodi hiyo, Msumi.
  “Mimi kama Mwenyekiti wa Yanga, natangaza kumfuta uanachama Msumi, ataitwa Kamati ya Maadili kujieleza. Na pia natangaza kuwafuta wanachama wale wote ambao sauti zao zimo humu,”amesema Manji.
  Pamoja na hayo, Manji akamuagiza Ofisa Habari wa klabu, Jerry Muro kupeleka sauti hizo Jeshi la Polisi Tanzania kwa ajili ya uchunguzi zaidi na awe anatoa taarifa kila wiki kulingana na mwendelezo wa uchunguzi.
  Aidha, Manji akasema anawafuta uanachama walke wote ambao wamechukua fomu za kugombea Yanga TFF. 
  Manji akasema kwamba Yanga inachukiwa na TFF kwa misimamo yake, ikiwemo kukataa baadhi ya mikataba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo inainyonya klabu hiyo.
  BARUA YA WAKILI KOMBA KUJITOA UCHAGUZI WA YANGA  Akadai na kwa sababu hiyo TFF wanafanya jitihada yeye aondoke Yanga ili wapate urahisi wa kupitisha Mikataba isiyo na maslahi na klabu.
  “Sisi tumetaka kujenga Uwanja wetu hapa (Jangwani), lakini tumehangaika na hatujapata sapoti yoyote ya TFF,”amesema.
  Manji akadai japokuwa watu wanalalamika Yanga inabebwa na TFF, lakini ukweli ni kwamba klabu hiyo inaonewa.
  “Tunapangiwa ratiba ngumu, tunacheza mechi bila kupumzika, wanataka Yanga ifungwe, ili Manji aambiwe ondoka, lakini tumechukua ubingwa, makombe yote, na Azam kabebwa ashiriki Kombe la Shirikisho,”amesema.
  “Tumewasaidia (Azam) ndugu zetu, si vibaya, lakini tulikuwa tuna uwezo wa kucheza mashindano yote ya Afrika. Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, ila kanuni haziruhusu,”amesema.
  Mvutano umeibuka kuhusu uchaguzi wa Yanga SC ambayo sasa inawaacha njia panda wanachaa wa klabu hiyo, wakiwa hawajui washike lipi baada ya TFF kutangaza na kuendesha mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo - wakati huo huo Yanga nayo ikitangaza na kuendesha mchakato yenyewe wa uchaguzi wake.
  Yanga imesema uchaguzi wake Yanga utafanyika Juni 11 na si Juni 25. TFF imenza kutoa fomu za kugombea Yanga mapema wiki hii, wakati klabu hiyo leo nayo imeanza kutoa fomu na Manji amekuwa mtu wa kwanza kuchukua, akifuatiwa na Makamu wake, Clement Sanga waliyekwenda pamoja. 
  Waliochukua fomu TFF ni Aaron Nyanda, Titus Osoro wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Paschal Laizer, Edgar Chibula, Mohammed Mattaka, Mchafu Ahmed Chakoma, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ Omari Said kutoka Zanzibar wanaowania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAKILI KOMBA WA TFF 'AWASUSIA' YANGA UCHAGUZI WAO KISA TUHUMA ZA MANJI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top