• HABARI MPYA

  Friday, June 03, 2016

  SAMATTA AWAAMBIA WATANZANIA; "NJOONI MUONE TUNAVYOCHINJA MAFARAO KESHO"

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Samatta amewakaribisha Watanzania kuishangilia timu yao ya taifa kesho dhidi ya Misri katika mchezo wa Kundi G kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), mwaka 2017 Gabon.
  Samatta aliyejiunga na kambi ya timu hiyo kwenye Hoteli ya Urban Rose, iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam, kabla ya kufanya na mazoezi na wenzake kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam aliwaambia waandishi wa habari na washindi wa promosheni ya Bia ya Kilimanjaro wanaodhamini timu hiyo kuwa shabiki ni mchezaji wa 12 katika kuleta hamasa ya ushindi.
  “Mimi ningependa kuwakaribisha mashabiki wote wa soka kuja uwanjani kwa ajili ya mchezo huu,” alisema Samatta ambaye ni nahodha wa Taifa Stars anayekipiga Klabu ya Genk ya Ubelgiji. Aliyasema hayo Jumatano jioni Juni 2, 2016 kabla ya mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya timu hiyo.
  Mbwana Ally Samatta amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kesho Uwanja wa Taifa

  Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, alisema kwamba kikosi chake kimekamilia kwa wachezaji wote kuwa katika ari ya mchezo na kwamba hakuna majeruhi yanayoweza kumzuia hata mmoja wa wachezaji wake kuitumikia timu yake hapo kesho.
  Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesikia kilio cha mashabiki wa soka, baada ya kutangaza viingilio kwa bei ya Sh 5,000 na Sh 10,000 kwa mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.00 jioni.
  Viingilio vilivyotangazwa ni Sh. 5,000 kwa mzunguko wenye viti vya Rangi ya Chungwa, Kijani na Bluu wakati Viti Maalumu vya alama “B” na “C” (VIP B na C),
  kiingilio ni Sh. 10,000.
  Tiketi hizo zitauzwa kwenye vituo vya Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam, Ukumbi wa Burudani Mbagala Dar Live, Vituo cha mafuta cha Oilcom - Ubungo na Buguruni (Buguruni Shell) na Ofisi za Ukumbi wa burudani Bilicanas.
  Kwa siku ya Jumamosi Juni 4, 2016 tiketi zitauzwa kwenye vituo hivyo vingine vya Mwenge, Mnazi Mmoja, Makumbusho, Chang’ombe na Mgahawa wa Brake Point ulioko mkabala makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
  Wakati huo huo: Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi, amepongeza uongozi wa timu ya Bunge FC uliochaguliwa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma.
  Viongozi waliochaguliwa ni Mwenyekiti Mhe. William Ngeleja (CCM); Makamu Mwenyekiti, Mhe. Esther Matiko; Meneja wa Klabu, John Kadutu pamoja Wajumbe ambao ni Mhe. Neema Mgaya, Mhe. Faida Bakari, Mhe. Cosato Chumi, Mhe. Anna Lupembe na Mhe. Grace Kihwelu.
  Rais Malinzi amewatakia kila la kheri Bunge Sports Club na kuwaahidi ushirikiano kutoka TFF katika kuendeleza klabu yao na michezo kwa ujumla.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA AWAAMBIA WATANZANIA; "NJOONI MUONE TUNAVYOCHINJA MAFARAO KESHO" Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top