• HABARI MPYA

    Tuesday, June 14, 2016

    PLUIJM AANZISHA PROGRAMU YA MAZOEZI YA USIKU YANGA KAMBI YA UTURUKI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    YANGA SC jana imeanza programu za mazoezi ya usiku, muda ambao ndiyo watacheza mechi yao ya kwanza ya Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Mouloudia Olympique Bejaia Juni 19, mwaka huu, Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria.
    Yanga imeweka kambi katika hotelki ya Rui mjini Antalya, Uturuki tangu juzi kujiandaa na mchezo unaosubiriwa kwa hamu.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana kwamba kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm sasa ameanzisha mazoezi ya usiku.
    Kocha wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm (katikati) akizungumza na wachezaji katika mazoezi ya usiku jana mjini Antalya, Uturuki

    “Na hii ni kwa sababu wapinzani wetu japo hawajatupa taarifa rasmi ya muda wa mechi, lakini tumekwishajua kwamba itakuwa usiku,”alisema Muro.
    Ofisa huyo alisema kwamba maandalizi yanaendelea vizuri na leo wanatarajia kumpokea beki Mtogo mwenye asili ya Ivory Coast, Vincent Bossou.
    Bossou hakuondoka na Yanga Dar es Salaam Alfajiri ya Jumapili kutokana kuchelewa kurejea nchini baada ya mapumziko kwa sababu ya kile alichoripoti, matatizo ya kifamilia.
    Na awali ilikuwa beki huyo aungane na timu moja kwa moja Algeria baada ya kumaliza matatizo yake ya kifamilia, lakini sasa anaiwahi kambi ya Uturuki hataiwahi.
    Yanga pia itamkosa beki wake tegemeo wa kulia, Juma Abdul aliyeumia kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) Mei 25 mwaka huu Yanga ikishinda 3-1 na akaenda kujitonesha akiichezea timu ya taifa, Taifa Stars ikifungwa 2-0 na Misri Juni 4, mwaka huu.
    Na kwa sababu hiyo, Juma Abdul anatakiwa kuwa nje kwa wiki mbili, hivyo beki mpya, Hassan Kessy anaweza kuanza mapema kuteleza upande wa kulia baada ya kusajiliwa mwezi uliopita kutoka kwa mahasimu, Simba SC.
    Mbali na Juma Abdul, wengine walioachwa niuhi Malimi Busungu, kipa Benedictor Tinocco na mshambuliaji Paul Nonga ambao hawamo kwenye programu ya kocha, wakati kinda Yussuf Mhilu hakwenda kwa sababu jina lake halijasajiliwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
    Kocha Pluijm akizungumza na wachezaji wake kuwapa maelekezo katika mazoezi ya Yanga usiku wa jana
    Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amekwenda lakini hatacheza mechi hiyo ya kwanza ya Kundi A kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi nyekundu, aliyopewa kwenye mchezo uliopita dhidi ya Sagrada Esperanca nchini Angola. 
    Kiungo Salum Telela ni mchezaji pekee aliyemaliza msimu na Yanga ambaye hajasafiri, kwa sababu hajapewa Mkataba mpya baada ya kumaliza wa awali.
    Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Morocco, Bouchaib El Ahrach atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Redouane Achik na Youssef Mabrouk.
    Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28 katika mchezo wake wa pili wa Kundi A.
    Na katika mchezo huo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa kutoka nchi tatu tofauti, ambao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O'michael wa Eritrea.
    Timu nyingine katika Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu, mchezo ambao utachezeshwa na marefa wa Shelisheli Bernard Camille, Hensley Danny Petrousse na Eldrick Adelaide.
    Kikosi kamili cha Yanga kilichopo kambini Uturuki ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya.
    Mabeki; Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' na Bossou anayetarajiwa kufika leo.
    Viungo; Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Godfrey Mwashiuya.
    Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony na Amissi Tambwe.
    Msafara upo chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa Mohammed Mpogolo na Meneja Hafidh Saleh. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PLUIJM AANZISHA PROGRAMU YA MAZOEZI YA USIKU YANGA KAMBI YA UTURUKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top