• HABARI MPYA

    Thursday, June 02, 2016

    MANJI: TFF NA BMT WANAFANYA NJAMA KUKATA JINA LANGU NISIGOMBEE YANGA, NINA USHAHIDI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Yanga, Yussuf Manji amechukua fomu za kutetea nafasi yake makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam leo na kudai kwamba kuna njama zinafanywa na baadhi ya watu ndani ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakate jina lake.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mchana Jangwani, Manji alidai kwamba alileta mpelelezi kutoka nje ya nchi akanasa mbinu hizo chafu hadi ushahidi wa sauti.
    Akasema katika sauti hizo wanasikika baadhi ya wanachama wa Yanga wakipanga njama kwa kushirikiana na watu wa TFF na BMT ili kukata jina lake katika uchaguzi.
    Akasema na hiyo ndiyo sababu hawana imani na TFF kuendesha uchaguzi wao na akasistiza Yanga itafanya yenyewe uchaguzi wake, tu kwa kusimamiwa na TFF.
    Manji akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani. Kulia ni Makamu wake, Clement Sanga
    Manji akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani. Kulia ni Makamu wake, Clement Sanga
    Manji akizungumza faragha na Makamu wake, Clement Sanga

    Pamoja na hayo, Manji ambaye aliwasikilizisha Waandishi wa Habari na wanachama waliokuwapo sauti hizo, akatangaza kumfuta uanachama, mwanachama ambaye sauti yake imevuma zaidi kwenye rekodi hiyo, Msumi.
    “Mimi kama Mwenyekiti wa Yanga, natangaza kumfuta uanachama Msumi, ataitwa Kamati ya Maadili kujieleza. Na pia natangaza kuwafuta wanachama wale wote ambao sauti zao zimo humu,”amesema Manji.
    Pamoja na hayo, Manji akamuagiza Ofisa Habari wa klabu, Jerry Muro kupeleka sauti hizo Jeshi la Polisi Tanzania kwa ajili ya uchunguzi zaidi na awe anatoa taarifa kila wiki kulingana na mwendelezo wa uchunguzi.
    Aidha, Manji akasema anawafuta uanachama walke wote ambao wamechukua fomu za kugombea Yanga TFF. 
    Manji akasema kwamba Yanga inachukiwa na TFF kwa misimamo yake, ikiwemo kukataa baadhi ya mikataba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo inainyonya klabu hiyo.
    Akadai na kwa sababu hiyo TFF wanafanya jitihada yeye aondoke Yanga ili wapate urahisi wa kupitisha Mikataba isiyo na maslahi na klabu.
    “Sisi tumetaka kujenga Uwanja wetu hapa (Jangwani), lakini tumehangaika na hatujapata sapoti yoyote ya TFF,”amesema.
    Manji akadai japokuwa watu wanalalamika Yanga inabebwa na TFF, lakini ukweli ni kwamba klabu hiyo inaonewa.
    “Tunapangiwa ratiba ngumu, tunacheza mechi bila kupumzika, wanataka Yanga ifungwe, ili Manji aambiwe ondoka, lakini tumechukua ubingwa, makombe yote, na Azam kabebwa ashiriki Kombe la Shirikisho,”amesema.
    “Tumewasaidia (Azam) ndugu zetu, si vibaya, lakini tulikuwa tuna uwezo wa kucheza mashindano yote ya Afrika. Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, ila kanuni haziruhusu,”amesema.
    Mvutano umeibuka kuhusu uchaguzi wa Yanga SC ambayo sasa inawaacha njia panda wanachaa wa klabu hiyo, wakiwa hawajui washike lipi baada ya TFF kutangaza na kuendesha mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo - wakati huo huo Yanga nayo ikitangaza na kuendesha mchakato yenyewe wa uchaguzi wake.
    Yanga imesema uchaguzi wake Yanga utafanyika Juni 11 na si Juni 25. TFF imenza kutoa fomu za kugombea Yanga mapema wiki hii, wakati klabu hiyo leo nayo imeanza kutoa fomu na Manji amekuwa mtu wa kwanza kuchukua, akifuatiwa na Makamu wake, Clement Sanga waliyekwenda pamoja. 
    Waliochukua fomu TFF ni Aaron Nyanda, Titus Osoro wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Paschal Laizer, Edgar Chibula, Mohammed Mattaka, Mchafu Ahmed Chakoma, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ Omari Said kutoka Zanzibar wanaowania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANJI: TFF NA BMT WANAFANYA NJAMA KUKATA JINA LANGU NISIGOMBEE YANGA, NINA USHAHIDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top