• HABARI MPYA

  Wednesday, June 22, 2016

  KIPIMO KINGINE CHA UBORA WA PLUIJM YANGA

  KATIKATI ya wiki ijayo, Yanga itacheza mechi yake ya pili ya Kundi A Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, itakapomenyana na Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Yanga itaingia kwenye mchezo huo na mabingwa hao mara tano Afrika ikitoka kufungwa 1-0 nchini Algeria na wenyeji MO Bejaia katika mchezo wa kwanza Jumapili.
  Na katika mchezo wa Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga itahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kwenda Nusu Fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani, baada ya Ligi ya Mabingwa.
  Yanga imeweka kambi nchini Uturuki, ambako iliweka kambi pia kabla ya mchezo na MO Bejaia.
  Na katika kambi yake ya Uturuki, umejitokeza mtihani mzito katika safu ya ulinzi, ambao ni mabeki wote wa kushoto kutokuwa katika nafasi ya kucheza.
  Wakati Mwinyi Hajji Mngwali atakuwa anatumikia adhabu yake kadi nyekundu aliyopewa katika mchezo wa Jumapili na MO Bejaia, baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano, Oscar Joshua ni majeruhi.
  Oscar ndiye aliyeanza Jumapili mjini Bejaia na akaumia kipindi cha kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na Mwinyi aliyekwenda kuonyeshwa kadi mfululizo za njano.
  Hadi jana hali ya Oscar ilikuwa si ya kumtarajia kuanza mazoezi wiki hii, maana yake uwezekano wa kucheza mechi ya Jumatano ijayo ni mdogo mno.
  Na ifahamike Mwinyi na Oscar ndiyo mabeki pekee wa kushoto kwenye kikosi cha Yanga na hakuna mchezaji ambaye anafikiriwa tofauti na wao anaweza kucheza upande huo.
  Huu ni mtihani mzito kwa Yanga kuelekea mchezo muhimu mno, ambao wanahitaji kushinda – na mbaya zaidi ni katika safu ya ulinzi.
  Huu ni wakati mwingine tena wa kocha Mholanzi wa Yanga, Hans van der Pluijm kutudhihirishia ubora wake kwa namna ambavyo anaweza kupata suluhisho la tatizo hilo.
  Miaka ya nyuma ndani ya Yanga zimewahi kutokea dharula kama hizo na makocha waliokuwapo waliwarudisha wachezaji wa mbele kucheza nafasi za ulinzi hatimaye wakageuka kuwa mabeki mahiri.
  Freddy Felix Minziro alisajiliwa Yanga mwanzoni mwa miaka ya 1980 kama winga, lakini baadaye akaja kuwa beki mahiri wa pembeni.
  John Alex Lwena alisajiliwa Yanga miaka ya 1980 kama winga kutoka Majimaji ya Songea, lakini baadaye akaja kuwa beki mahiri wa kulia.
  Mwanamtwa Mussa Kihwelo alisajiliwa Yanga kutoka Reli ya Morogoro mwaka 1992 kama kiungo wa ulinzi, lakini baadaye akaja kuwa beki tegemeo wa kulia.
  Fredy Mbuna Swale alisajiliwa Yanga mwaka 2000 kama mshambuliaji, lakini akastaafu miaka 10 baadaye kama beki wa kulia.  
  Na wote walikuwa wanarudishwa kucheza nafasi za ulinzi baada ya kutokea dharula ya kukosekana mtu mwingine wa kucheza.
  Mfano Mtwa Kihwelo, mwaka 1993 Yanga ilikuwa Kampala, Uganda kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati na David Mwakalebela aliyesajiliwa kwa ajili ya nafasi hiyo kutoka Pamba ya Mwanza akachemsha katika mchezo wa kwanza dhidi ya SC Villa, Yanga ikafungwa 3-0. 
  Mchezo uliofuata aliyekuwa kocha wa Yanga, Mrundi Nzoyisaba Tauzany ‘Bundes’ (sasa marehemu) akampanga Mtwa beki ya kulia akacheza hadi fainali Yanga ikichukua Kombe kwa kuwafunga hao hao Villa 2-1.
  Bundes pia alimtoa Issa Athumani (sasa marehemu) nafasi ya kiungo na kumpanga sentahafu, baada ya Salum Kabunda (sasa marehemu) kugoma kwenda Uganda akisema amechoka kutokana na kucheza timu ya taifa katika Kombe la Challenge mwezi uliotangulia.
  Na ukitazama kikosi cha Yanga cha sasa, ukiondoa uhaba wa watu wa nafasi za ulinzi, idara nyingine zote zina watu zaidi ya mmoja – ndiyo maana ninasema ni wakati mwingine wa Pluijm kutudhihirishia ubora wake, tunataka tuone atafanya nini kukabiliana na hali iliyopo? 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIPIMO KINGINE CHA UBORA WA PLUIJM YANGA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top