• HABARI MPYA

    Monday, June 13, 2016

    BOSSOU KUUNGANA NA YANGA KESHO UTURUKI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BEKI wa kati wa Yanga, Mtogo mwenye asili ya Ivory Coast, Vincent Bossou atajiunga na wenzake kesho kambini nchini Uturuki.
    Yanga imeweka kambi katika hotelki ya Rui mjini Antalya, Uturuki kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mouloudia Olympique Bejaia Juni 19, mwaka huu, utakaofanyika Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria.
    Bossou hakuondoka na Yanga Dar es Salaam Alfajiri ya jana kutokana kuchelewa kurejea nchini baada ya mapumziko kwa sababu ya kile alichoripoti, matatizo ya kifamilia.
    Na awali ilikuwa beki huyo aungane na timu moja kwa moja Algeria baada ya kumaliza matatizo yake ya kifamilia, lakini sasa ataiwahi kambi ya Uturuki hataiwahi.
    Vincent Bossou ataungana na kikosi cha Yanga kesho nchini Uturuki

    Yanga pia itamkosa beki  wake tegemeo wa kulia, Juma 
    Abdul aliyeumia kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) Mei 25 mwaka huu Yanga ikishinda 3-1 na akaenda kujitonesha akiichezea timu ya taifa, Taifa Stars ikifungwa 2-0 na Misri Juni 4, mwaka huu.
    Na kwa sababu hiyo, Juma Abdul anatakiwa kuwa nje kwa wiki mbili, hivyo beki mpya, Hassan Kessy anaweza kuanza mapema kuteleza upande wa kulia baada ya kusajiliwa mwezi uliopita kutoka kwa mahasimu, Simba SC.
    Mbali na Juma Abdul, wengine walioachwa niuhi Malimi Busungu, kipa Benedictor Tinocco na mshambuliaji Paul Nonga ambao hawamo kwenye programu ya kocha, wakati kinda Yussuf Mhilu hatakwenda kwa sababu jina lake halijasajiliwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
    Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amesafiri lakini hatacheza mechi hiyo ya kwanza ya Kundi A kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi nyekundu, aliyopewa kwenye mchezo uliopita dhidi ya Sagrada Esperanca nchini Angola. 
    Kiungo Salum Telela ni mchezaji pekee aliyemaliza msimu na Yanga ambaye hatasafiri, kwa sababu hajapewa Mkataba mpya baada ya kumaliza wa awali.
    Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Morocco, Bouchaib El Ahrach atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Redouane Achik na Youssef Mabrouk.
    Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28 katika mchezo wake wa pili wa Kundi A.
    Na katika mchezo huo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa kutoka nchi tatu tofauti, ambao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O'michael wa Eritrea.
    Timu nyingine katika Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu, mchezo ambao utachezeshwa na marefa wa Shelisheli Bernard Camille, Hensley Danny Petrousse na Eldrick Adelaide.
    Kikosi kamili cha Yanga kinachokwenda Uturuki ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya.
    Mabeki; Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.
    Viungo; Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Godfrey Mwashiuya.
    Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony na Amissi Tambwe.
    Msafara umeongozwa na Kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa Mohammed Mpogolo na Meneja Hafidh Saleh. Safari njema Yanga. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BOSSOU KUUNGANA NA YANGA KESHO UTURUKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top