• HABARI MPYA

    Tuesday, August 06, 2019

    SIMBA SC YAICHAPA POWER DYNAMOS 3-1, MEDDIE KAGERE AANZA MSIMU NA HAT TRICK

    Na Asha Said, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imezindua vyema msimu wake mpya baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia katika mchezo wa kirafiki kwenye tamasha la Simba Day usiku wa leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo uliokusanya umati wa mashabiki waliosheheni Uwanja wa Taifa, shujaa wa Simba SC alikuwa ni mshambuliaji wake wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere aliyefunga mabao yote matatu ya timu yake.
    Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa wa kike wa kimataifa wa Tanzania, Jeonesya Rukyaa, hadi mapumzuiko timu hizo zilikuwa zimefungana 1-1.

    Alianza Kagere kuwafungia Wekundu wa Msimbazi dakika ya tatu tu ya mchezo, akimalizia pasi ya kiungo Mzambia, Clatous Chama, kabla ya Jimmy Dlingai kuisawazishia Power Dynamos kwa kichwa dakika ya 23 akimalizia kona iliyopigwa na Larry Bwalya kumtungua kipa wa zamani wa Yanga, Beno Kakolanya.
    Kipindi cha pili Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems ikarejea na moto zaidi na kupata mabao mawili zaidi, yote yakifungwa na Kagere ‘Terminator’ .
    Alianza kufunga dakika ya 58 kwa kichwa akimalizia pasi ya winga mpya, Deo Kanda aliyesajiliwa kutoka TP Mazembe ya kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na dakika ya 73 kwa shuti akimalizia kona ya Chama.
    Baada ya mchezo huo, Simba SC watasafiri kwenda Msumbiji kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, UD do Songo Jumamosi, kabla ya kurejea nyumbani kwa mchezo wa marudiano kati ya Agosti 23 na 25.
    Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza, Simba itakutana na mshindi kati ya FC Platinum ya Zimbabwe na Nyasa Bullets ya Malawi na ikifuzu mtihani huo pia itaingia tena hatua ya makundi.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Beno Kakolanya, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Shomary Kapombe/Said Ndemla dk85, Tairon Santos Da Silva/Kennedy Juma dk87, Pascal Wawa, Muzamil Yassin, Deo Kanda/Rashid Juma dk75, Sharaf Eldin Shaibob/Gerson Fraga ‘Viera’ dk49, Meddie Kagere, Clatous Chama na Francis Kahata/Miraj Athumani ‘Madenge’ dk61.
    Power Dynamos; Lawrence Mulenga, Larry Bwalya, Raphael Makubuli, Jimmy Dlingai, John Soico/Clifford Saudi dk75, White Mwamambaba, Benson Sakala, Kondwani Chiboni/Faustin Bakodica dk51, Christian Ntouba/Judo Bolondio dk59, Fredrick Mulamba/Jackob Phiri dk54 na Kassimu Titus/Lameck Kafwaya dk67.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAICHAPA POWER DYNAMOS 3-1, MEDDIE KAGERE AANZA MSIMU NA HAT TRICK Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top