• HABARI MPYA

    Sunday, August 04, 2019

    SAMATTA AFUNGA BAO LA KWANZA LA MSIMU LAKINI KRC GENK YACHAPWA 3-1 UBELGIJI

    Na Mwandishi Wetu, GENK
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana amefunga bao lake la kwanza la msimu, lakini bahati mbaya timu yake imechapwa 3-1 na wenyeji, KV Mechelen katika mchezo wa pili tu wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji.
    Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa AFAS- Achter de Kazerne mjini Mechelen, Malines, Samatta alifunga dakika ya dakika ya 45 na ushei akimalizia pasi ya kiungo Mbelgiji, Bryan Heynen.
    Na hilo lilikuwa bao la kusawazisha baada ya KV Mechelen kutangulia kwa bao la Muivory Coast, William Togui dakika ya 18, kabla ya washambuliaji wenzake, Msweden Gustav Engvall kufunga la pili dakika ya 77 na Mbrazil, Igor Alberto de Camargo kufunga la tatu dakika ya 80.


    Ushindi huo ni sawa na kulipa kisasi kwa Mechelen baada ya kuchapwa 3-0 kwenye mchezo wa Super Cup Julai 20 Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
    Ikumbukwe mchezo wa kwanza wa msimu, Genk ilianza vyema ushindi wa 2-1 dhidi ya Kortrijk Uwanja wa Luminus Arena.
    Jana Samatta  mwenye umri wa miaka 26 sasa, ameifungia Genk bao la 63 katika mechi 158 za mashindano yote tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Katika ligi ya Ubelgiji pekee amefunga mabao 48 sasa katika mechi 124, kwenye Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa, Super Cup mechi moja na Europa League amefunga mabao 14 katika mechi 24.
    Kikosi cha KV Mechelen kilikuwa: Thoelen, Bijker, Van Cleemput, Swinkels, Kaya, Togui/De Camargo dk71, Storm, Van Damme/Corryn dk22, Schoofs, Engvall/Bateau dk88 na Peyre.
    KRC Genk: Coucke, Uronen, Dewaest, Cuesta, Maehle, Berge, Heynen, Nygren/Hagi dk45, Paintsil/Odey dk82, Ito/Benson dk72 na Samatta.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA AFUNGA BAO LA KWANZA LA MSIMU LAKINI KRC GENK YACHAPWA 3-1 UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top