• HABARI MPYA

  Friday, March 02, 2018

  SIMBA SC YAVUTWA MKIA, SARE 3-3 NA STAND UNITED TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imepunguzwa kasi baada ya sare ya kufungana mabao 3-3 na Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Sare hiyo inaiongezea kila timu pointi moja, Simba SC wakifikisha pointi 46 baada ya mechi 20 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ikiwazidi pointi sita mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 40 za mechi 19, wakati Stand inafikisha pointi 21 sasa baada ya kucheza mechi 20 na kupanda kwa nafasi mbili hadi nafasi ya nane.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Florentina Zabron wa Dodoma aliyesaidiwa na Ferdinand Chacha na Mashaka Mandemwa wote wa Mwanza hadi mapumziko kila timu iliondoka na uwanjani na mabao mawili. 
  Beki Mghana wa Simba, Asante Kwasi akijaribu kupasua katikati ya wachezaji wa Stand United leo Bigirimana Blaise (kulia) na Aaron Lulambo (kushoto) 
  Mshambuliaji wa Stand United, Vitalis Mayanga (kulia) akiuwahi mpira dhidi ya kiungo wa Simba, Muzail Yassin 
  Mshambuliaji Simba, Laudit Mavugo akimtoka Mrundi mwenzake, Bigirimana Blaise   
  Mshambuliaji Mghana wa Simba, Nicholaus Gyan (kulia) akiwania mpira wa juu dhidi ya Ally Ally (kushoto) wa Stand United 

  Simba SC walitangulia kwa mabao ya beki Mghana, Asante Kwasi dakika ya sita akimalizia mpira uliotemwa na kipa Mohammed Makaka baada ya shuti la mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo.
  Mrundi Mavugo aliye katika msimu wa pili Msimbazi tangu asajiliwe kutoka Vital’O ya kwao, akaifungia Simba bao la pili dakika ya 23 akimalizia krosi ya beki wa kulia, Shomary Kapombe.
  Safu ya ulinzi ya Simba ikapatwa na ukakasi na kujikuta inaruhusu mabao mawili rahisi na kwenda kupumzika wakiwa wamefungana 2-2 na timu ya Shinyanga, maarufu kama ‘Chama la Wana’.
  Tariq Seif alifunga kwa kichwa dakika ya 36 akimalizia krosi ya Aaron Lulambo ambaye naye alifunga la pili dakika ya 40 kufuatia kona yake kuingia moja kwa moja nyavuni.
  Kipindi cha pili, Simba walikianza na mabadiliko wakimpumzisha Mavugo aliyemaliza kipindi cha kwanza anachechemea baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na mzawa, Juma Luizio. 
  Mabadiliko hayo yaliisaidia Simba kupata bao la tatu lililofungwa na mshambuliaji Mghana, Nicholaus Gyan kwa shuti akiwa ndani ya boksi dakika ya 61 kufuatia mabeki wa Stand United kuzembe kuokoa mpira wa kona iliyochongwa na Muzamil Yassin.
  Ikawachukua dakika tano tu Stand kusawazisdha tena, mfungaji Mrundi Bigirimana Blaise dakika ya 67 kwa shuti kali kufuatia mpira wa kurushwa na beki wa kushoto, Miraj Maka.
  Simba inarejea kambini baada ya mechi ya leo kujiandaa na mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika Jumatano dhidi ya El Masry ya Misri.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Asante Kwasi, Yussuf Mlipili, James Kotei, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Muzamil Yassin/Mwinyi Kazimoto dk74, Laudit Mavugo/Juma Luizio dk46, Shiza Kichuya na Nicholas Gyan/Moses Kitandu dk90+2.
  Stand United; Mohamed Makaka, Aaron Lulambo, Miraj Maka, Erick Mulilo, Ally Ally/Abdallah Juma dk90, Abel Kassim/Ismail Gambo dk81, Bigirimana Blaise/Sixtus Sabilo dk70, Jisendi Mathias, Tariq Seif, Suleiman Ndikumana na Vitalis Mayanga.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAVUTWA MKIA, SARE 3-3 NA STAND UNITED TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top