• HABARI MPYA

    Friday, November 10, 2017

    SAMATTA AFANYIWA UPASUAJI KWA SAA MOJA UBELGIJI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amefanyiwa upasuaji wa goti leo mjini Genk, Ubelgiji baada ya kuumia wiki iliyopita na sasa anaanza safari ya kuishi wiki sita na zaidi bila kufanya mazoezi.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Samatta amesema kwamba upasuaji huo ulidumu kwa saa moja na baada ya hapo akarejea nyumbani kwake kwa kiti maalum cha kutembelea walevamu, au wagonjwa wasiojiweza kutembea.
    “Napenda kuwajulisha kuwa operesheni yangu imeenda vizuri. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, timu ya madaktari pamoja na mashabiki wangu. Nimepokea meseji nyingi sana kutoka sehemu tofauti duniani na napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana kwa meseji na dua zenu,”amesema Samatta.
    Mbwana Samatta amefanyiwa upasuaji kwa saa moja leo mjini Genk baada ya kuumia wiki iliyopita


    Samatta aliumia goti Jumamosi ya Novemba 4, mwaka huu akiichezea klabu yake, KRC ikilazimishwa sare ya 0-0 Jumamosi na Lokeren katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
    Na baada ya kufanyiwa vipimo ikagundulika Samatta ameumia kwenye mishipa midogo ya goti lake la mguu wa kulia ambayo ilichanika, hivyo kuhitaji kufanyiwa upasuaji mdogo ili apone sawia.
    Samatta aliumia akiichezea mechi ya 70 Genk tangu alipojiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Na katika mechi hizo 70, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mashindano yote.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA AFANYIWA UPASUAJI KWA SAA MOJA UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top