• HABARI MPYA

    Tuesday, November 28, 2017

    SIMBA SC WAPEWA SIKU NNE MAPUMZIKO, KUREJEA IJUMAA MAZOEZINI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WACHEZAJI wa Simba wamepewa mapumziko ya siku nne tu hadi Ijumaa kabla ya kurudi kuendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi zao zijazo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Ligi Kuu inatarajiwa kusimama kwa wiki mbili hadi tatu kupisha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge na wachezaji kadhaa wa Simba wanakwenda kujiunga na timu zao za taifa.
    Simba inakwenda kupumzika ikiwa bado inaongoza Ligi Kuu licha ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Lipuli ya Iringa Jumapili Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Wachezaji wa Simba wakimpongeza Mwinyi Kazimoto (kushoto) baada ya kufunga bao zuri la kuongoza

    Simba SC inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 23 baada ya mechi 11, ikiwazidi kwa pointi mbili tu mabingwa watetezi, Yanga ambao nao Jumamosi walilazimishwa sare ya 1-1 na Tanzania Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Katika mchezo wa jumapili uliochezeshwa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, aliyesaidiwa na Khalfan Sika wa Pwani na Vincent Mlabu wa Morogoro iliwachukua dakika 15 tu Simba kupata bao la kuongoza, lililofungwa na kiungo wake mkongwe, Mwinyi Kazimoto Mwitula.
    Kazimoto alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi ya kiungo mwenzake, Muzamil Yassin mbele ya mstari wa kuugawa Uwanja na kutembea nayo hatua mbili kabla ya kumtungua kwa mpira wa juu kipa wa Lipuli, Agathony Mkwando aliyetokea kujaribu kuokoa. 
    Simba ilipata bao hilo ikitoka kupoteza nafasi tatu nzuri za kufunga mabao kupitia kwa nyota wake John Bocco, Shiza Kichuya na Muzamil Yassin.
    Lipuli walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika nne baadaye kupitia kwa Nahodha wao, Mghana Asante Kwasi aliyefunga kwa shuti la mpira wa adhabu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAPEWA SIKU NNE MAPUMZIKO, KUREJEA IJUMAA MAZOEZINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top