• HABARI MPYA

    Wednesday, November 29, 2017

    KIPA WA YANGA, KINDA WA AZAM WAONGEZWA KILI STARS

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Stars’, Ammy Conrad Ninje, ameongeza nyota watatu katika kikosi chake mara baada ya Baraza la Soka la Afrika Mashariki (CECAFA), kuridhia kuongezwa wachezaji watatu kwa kila timu.
    Awali, CECAFA ilihitaji wachezaji 20 tu, lakini sasa wameongeza watatu na kufanya idadi mpya ya wachezaji watakaoshiriki michuano hiyo ya Chalenji kwa mwaka huu kuwa 23.
    Wachezaji walioongezwa na Kipa Ramadhani Kabwili kutoka Young Africans ya Dar es Salaam, Amani Kiata  wa Nakuru All Stars ya Kenya na Yahya Zayed kutoka Azam FC ya Dar es Salaam.
    Kipa wa tatu wa Yanga, Ramadhani Kabwili ameongezwa Kilimanjaro Stars
    Kikosi cha wachezaji 20 wa awali wa Ninje - Kocha wa Daraja ‘A’ la Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), ni makipa Aishi Manula (Simba SC) na Peter Manyika (Singida United).
    Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphace Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Kennedy Juma (Singida United), Erasto Nyoni (Simba SC) na Mohammed Hussein (Simba SC).
    Viungo wa kati ni Himid Mao ambaye ni Nahodha (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Mzamiru Yassin (Simba SC), Raphael Daud (Young Africans), Shizza Kichuya (Simba SC), Abdul Hilal (Tusker/Kenya) na Ibrahim Ajib (Young Africans).
    Washambuliaji ni Mbaraka Yussuph (Azam FC), Elias Maguri (Dhofar/Mascat, Oman), Daniel Lyanga (Fanja FC/Mascat) na Yohana Mkomola (Ngorongoro Heroes). 
    Benchi la Ufundi linaundwa na yeye Ninje ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa). 
    Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Desemba 3, mwaka huu, Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi ‘A’ pamoja wenyeji Kenya, Rwanda na Libya ambayo ni timu mwalikwa kutoka Kaskazini mwa Afrika.
    Kilimanjaro Stars ambayo imewahi kutwaa mara tatu taji hilo la Chalenji tangu kuanzishwa kwake, itaaza kampeni za kurudisha heshima yake dhidi ya Libya katika kundi hilo la A utaofanyika Desemba 3, mwaka huu.
    Mashindano ya mwaka huu CECAFA ilifikia makubaliano na kanda mbili za Kusini mwa Afrika - COSAFA na ile ya Kaskazini UNAF kualika timu mbili za kutoka kanda hizo na mataifa ya Libya na Zimbabwe.
    Jumla ya timu shiriki kwenye CECAFA Senior Challenge Cup mwaka huu itakuwa 10 ambazo ni pamoja na wenyeji Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, South Sudan, Ethiopia, Zanzibar, Somalia, Zimbabwe na Libya. 
    Sudan wenyewe wamejiondoa katika mashindano ya mwaka huu wakati mataifa mawili ya Eritrea na Djibouti nayo hayatashiriki.
    Michuano hiyo itatumia viwanja vya Moi kilichopo Kisumu (Moi Stadium), Bukungu kilichopo Kakamega na Afraha kilichopo Nakuru wakati Uwanja wa Kasarani Nairobi na ule wa Kenyatta uliopo Machakos vitatumika kama viwanja vya ziada.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPA WA YANGA, KINDA WA AZAM WAONGEZWA KILI STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top