• HABARI MPYA

  Friday, November 10, 2017

  MECHI YA STARS NA BENIN ITAKUWA ‘LIVE’ AZAM TV JUMAPILI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MCHEZO wa kirafiki wa kimataifa kati ya wenyeji, Benin na Tanzania Jumapili Uwanja wa l'Amitie, au Urafiki mjini Cotonou utaonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV.
  Mkurugenzi wa Michezo wa AzamTV, Patrick Kahemele amesema kwamba mchezo huo utaonyeshwa na chaneli ya Azam Sports 2 kuanzia Saa 12:00 jioni kwa saa za Tanzania.
  Taifa Stars inayofundishwa na Salum Mayanga, akisaidiwa na Fulgence Novatus, Amy Ninje na Patrick Mwangata wote wachezaji wa zamani nchini, chini ya Meneja, Danny Msangi, iliwasili mjini Cotonou jana tayari kwa mchezo huo ulio kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
  Kipa Peter Manyika na beki Abdi Banda wakiwa kwenye ndege wakati wa safari ya Benin jana

  Kikosi cha Taifa Stars kilichowasili Cotonou kwa ajili ya mchezo huo, kinaundwa na makipa; Aishi Manula  wa Simba SC, Peter Manyika wa Singida United na Ramadhani Kabwili wa Yanga SC.
  Mabeki ni Boniphace Maganga wa Mbao FC, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Gardiel Michael, Kevin Yondan wa Yanga, Nurdin Chona wa Tanzania Prisons na Dickson Job wa Mtibwa Sugar.
  Viungo ni Himid Mao wa Azam FC, Mudathir Yahya wa Singida United, Hamisi Abdallah wa Sony Sugar ya Kenya, Jonas Mkude, Shiza Kichuya wa Simba, Ibrahim Hajib, Raphael Daudi wa Yanga, Simon Msuva wa Difaa Hassan El Jadida wa Morocco, Mohammed Issa wa Mtibwa Sugar, Farid Mussa wa Tenerife B ya Hispania na Abdul Mohammed wa Tusker ya Kenya.
  Washambuliaji ni Mbaraka Yussuf wa Azam FC, Elias Maguri na Yohanna Nkomola ambao wote hawana timu kwa sasa.
  Nahodha Mbwana Samatta alienguliwa kikosini mapema wiki hii baada ya kuumia akiichezea klabu yake, KRC Genk katika Ligi ya Ubelgiji na atakuwa nje kwa miezi miwili.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MECHI YA STARS NA BENIN ITAKUWA ‘LIVE’ AZAM TV JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top