• HABARI MPYA

    Wednesday, November 29, 2017

    NINJE APEWA NAFASI YA KUONGEZA WATATU KIKOSI CHA CHALLENGE

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limempa fursa kocha Ammy Ninje kuongeza wachezaji watatu kwenye kikosi cha timu ya Bara kitakachoshiriki Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwaka huu.
    Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba wamemuambia kocha Ninje aongeze wachezaji watatu akitaka kufuatia Baraza la Vyama na Mashirikisho ya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kuzipa nafasi hiyo Uganda na Rwanda.
    Uganda na Rwanda zinatarajiwa kucheza fainali za ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) Januari mwakani zinazohusisha wachezaji wanaocheza Ligi za nchini mwao pekee na katika kuwawezesha kuviandaa vikosi vyao vyote, CECAFA imewapa nafasi Amavubi na The Cranes kwenda na wachezaji 23.
    Wachezaji wa Kilimanjaro Stars wakiwa mazoezini jana Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam

    “Sasa baada ya kuzipa nafasi hiyo ya upendeleo Rwanda na Uganda, CECAFA pia ikasema kwa nchi nyingine zitakazoweza kuongeza wachezaji watatu kwa gharama zao wenyewe zinaruhusiwa. Nasi kwa sababu hiyo tumempa fursa hiyo mwalimu, sasa ni jukumu lake mwenyewe kuongeza au la,”amesema Kidau, kiungo wa zamani wa Milambo, Simba na Vijana ya Ilala ‘Kabakayeka’.   
    Kikosi cha Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kinatarajiwa kuondoka Dar es Salaam kesho baada ya mazoezi ya siku tatu kwenda nchini Kenya, ambako michuano ya CECAFA Challenge inatarajiwa kufanyika kuanzia Desemba 3 hadi 16, mwaka huu. 
    Wachezaji wote walioteuliwa wapo kambini kasoro Daniel Lyanga wa Fanja ya Oman, ambaye anatarajiwa kuwasili leo.
    Kikosi kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Simba SC) na Peter Manyika (Singida United).  
    Mabeki ni Boniphace Maganga (Mbao FC), Gardiel Michael (Yanga SC), Kelvin Yondani (Yanga SC), Erasto Nyoni (Simba SC), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba SC) na Kennedy Wilson (Singida United).
    Viungo ni Himid Mao (Azam FC), Hamisi Abdallah (Sony Sugar- Kenya), Muzamil Yassin (Simba SC), Raphael Daudi (Yanga SC), Jonas Mkude (Simba), Shiza Kichuya (Simba SC), Ibrahim Ajib (Yanga) na Abdul Hilal (Tusker FC - Kenya).
    Washambuliaji ni Elias Maguri (huru), Mbaraka Yusuph (Azam FC), Yohana Nkomola (huru) na Daniel Lyanga (Fanja FC, Oman).
    Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi A pamoja na ndugu zao, Zanzibar, wenyeji Kenya, Rwanda na waalikwa Libya, wakati Kundi B lina timu za Uganda, Zimbabwe, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini.
    Kilimanjaro Stars itafungua dimba na Libya Desemba 3, mwaka huu mchezo ambao utafuatiwa na mechi kati ya wenyeji, Kenya dhidi ya Rwanda.
    Kili Stars itarudi uwanjani Desemba 7 kumenyana na Zanzibar Heroes, Desemba 9  na Rwanda kabla ya kumaliza mechi zake za Kundi A kwa kumenyana na wenyeji, Kenya Desemba 11.
    Mechi za makundi zinatarajiwa kukamilishwa Desemba 12 na Nusu Fainali zitachezwa Desemba 14 na 15, wakati Desemba 16 itachezwa mechi ya kusaka mshindi wa tatu ikifuatiwa na fainali.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NINJE APEWA NAFASI YA KUONGEZA WATATU KIKOSI CHA CHALLENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top