• HABARI MPYA

    Wednesday, November 22, 2017

    AZAM FC YAMSAINISHA MSHAMBULIAJI MWINGINE KUTOKA GHANA

    Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Azam FC imemsajili imemsajili mshambuliaji mwingine Mghana, Bernard Arthur kutoka klabu ya Liberty Professional ya Ghana.
    Arthur amesaini mkataba wa miaka miwili kujiaunga na matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, na zoezi zima limefanikishwa na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohammed, aliyekuwepo nchini Ghana kukamilisha usajili wake.
    Usajili wa Arthur, 20, ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi la timu hiyo kwenye usajili huu wa dirisha dogo, anayekuja kuziba pengo la straika mwingine, Yahaya Mohammed, aliyeondoka kwa makubaliano maalumu ya pande mbili wiki chache zilizopita.
    Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohammed (kulia) akimkabidhi jezi ya klabu mshambuliaji Bernard Arthur kutoka klabu ya Liberty Professional ya Ghana 
    Mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya WAFA (Ghana) na Asec Mimosa ya Ivory Coast, anaungana na washambuliaji wengine wa timu hiyo katika kukiongezea makali kikosi hicho, ambao ni Mbaraka Yusuph, Wazir Junior, Yahya Zayd, Shaaban Idd pamoja na wale waliopandishwa kutoka Azam B, Paul Peter na Andrea Simchimba.
    Liberty Professional ni moja ya kitovu kikubwa cha kutoa mastaa wa baadaye nchini Ghana, wachezaji waliotesa barani Ulaya waliowahi kupiatia hapo ni nyota wa zamani wa Chelsea, Michael Essien, Sulley Muntari (Pescara, Italia) na Asamoah Gyan (Kayserispor, Uturuki).
    Azam FC inamatumaini makubwa kuwa usajili wa nyota huyo, utaweza kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji na kutatua tatizo la ukosefu wa mabao linaloonekana, hii ikitarajia kuendeleza mbio za kuwania taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania walizozianza vema hadi sasa.
    Aidha uongozi kwa ujumla na Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC, unaendelea kutoa pongezi kwa mashabiki wa timu kwa moyo wanaoendelea nao wa kuisapoti timu hiyo, kwa hakika kila mmoja amejionea namna nguvu na umoja wao wa kuishangilia timu unavyozidi kuwapa hamasa wachezaji na kupata matokeo bora kwenye kila mchezo.
    Arthur aliyekuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya vijana ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 (Ghana U-20), ni mmoja wa washambuliaji bora kwa sasa katika Ligi Kuu nchini Ghana (GPL), msimu huu akifunga jumla ya mabao 11, tisa akifunga ndani ya ligi hiyo na mawili (Kombe la FA).
    Moja ya sifa zake kubwa ni uwezo wa kumiliki mpira na kuwatoka mabeki wa timu pinzani kwa spidi, kukaa na mipira na kusambaza kwa wachezaji wenzake, kutumia vizuri miguu yote miwili, uwezo wa kupiga mashuti kwenye eneo lolote la ushambuliaji pamoja na kusaidia ukabaji pale timu pinzani inapokuwa ikishambulia.
    Arthur alianzia soka lake katika timu ya Mighty Cosmos kwenye eneo alilozaliwa na kukulia la Dansoman nchini Ghana, akiwa kijana mdogo mwaka 2005-2010.
    Cosmos aliyoanzia soka lake Arthur, pia wamewahi kucheza nyota wengi wa soka la Ghana wakiwamo nahodha wa zamani na timu ya Taifa ‘Black Star’, Stephen Appiah na Michael Essien.
    Mbali na kucheza Liberty, mshambuliaji huyo pia amewa kucheza kwa mabingwa wa msimu uliopita nchini Ghana, WAFA huku pia akiwahi kutolewa kwa mkopo kujiunga kwa vigogo wa Ivory Coast, Asec Mimosa.
    Nyota huyo anavutiwa na staa wa Ghana, Asamoah Gyan, ambaye ndiye mfano wake wa kuigwa (role model), ambapo anapenda siku moja wacheze naye pamoja katika timu Taifa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAMSAINISHA MSHAMBULIAJI MWINGINE KUTOKA GHANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top