• HABARI MPYA

    Wednesday, November 22, 2017

    TSHISHIMBI TATIZO JIPYA YANGA, TAMBWE AONYESHA MATUMAINI

    Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
    WAKATI mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe amefanya mazoezi kikamilifu kwa mara ya kwanza leo baada ya muda mrefu, kuna uwezekano Yanga SC ikaendelea kumkosa kiungo wake, Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi.
    Tshishimbi hakuwepo wakati Yanga SC inaifunga 5-0 Mbeya City Jumapili iliyopita Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Na kuelekea mchezo ujao dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Tshishimbi kwa mara nyingine tena leo ameshindwa kuanza mazoezi.
    Kocha wa Yanga, Mzambia George ‘GL’ Lwandamina amesema kwamba kati ya majeruhi wake wanne, wengine Wazimbabwe kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji, Donald Ngoma ni Tambwe pekee amefanya mazoezi leo.
    Yanga SC ikaendelea kumkosa kiungo wake, Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi (kulia)

    Tambwe alifanya mazoezi mepesi ya kukimbia peke yake juzi na jana Uwanja wa Uhuru, kabla ya leo kuungana na wenzake kwa program kamili ya mazoezi.
    Lwandamina amesema kwamba inaonekana Tambwe amerudi imara kabisa na leo alionyesha yuko fiti kwa kucheza kwa nguvu na kupiga mashuti ya kusisimua.    
    Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itaendelea Ijumaa, wenyeji Ndanda FC wakiwakaribisha Njombe Mji FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Jumamosi, Yanga wataikaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na  Singida United watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Namfua, Singida.
    Mechi nyingine za jumamosi, Mbao FC wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Kagera Sugar wataikaribisha Stand United Uwanja wa kambarage Shinyanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Maji Maji Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. 
    Jumapili Simba SC watakuwa wenyeji wa Lipuli ya Iringa Uwanja wa Azam, Complex na mzunguko wa 11 wa Ligi Kuu inayoonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV utakamilishwa Jumatatu ijayo kwa mchezo mmoja kati ya wenyeji, Azam FC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TSHISHIMBI TATIZO JIPYA YANGA, TAMBWE AONYESHA MATUMAINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top