• HABARI MPYA

    Sunday, May 21, 2017

    NIYONZIMA, MWANJALI KUCHUANA NA NDIKUMANA MCHEZAJI BORA WA KIGENI LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIUNGO wa Rwanda, Haruna Niyonzima anayechezea Yanga, atachuana na beki Mzimbabwe anayechezea Simba, Method Mwanjali na kiungo Mrundi, Yussuf Ndikumana wa Mbao FC katika kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Sherehe na Vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inatarajiwa kufanyika Mei 24 mwaka huu ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam.
    Kamati Maalum iliyoundwa kusimamia tuzo hiyo imefanya mabadiliko kiasi kwa kuongeza baadhi ya tuzo ambazo hazikuwepo msimu uliopita lengo ikiwa ni kuboresha tuzo.
    Tuzo zilizoongezwa ni: Tuzo ya Heshima (ambayo itatolewa kwa mwanasoka nguli wa zamani mwenye historia nzuri kwa soka la Tanzania).
    Haruna Niyonzima (kushoto) akifanya moja ya vitu vilivyomuingiza fainali ya Mchezaji Bora wa kigeni Ligi Kuu

    Nyingine  ni: Tuzo ya Kikosi Bora cha Msimu (Itatolewa kwa wachezaji Bora 11 wa Ligi Kuu (VPL XI 2016/2017) walioteuliwa kutokana na ufanisi wao katika ligi hiyo msimu huu.
    Pia imeongezwa Tuzo ya Mchezaji Bora mwenye chini ya umri wa miaka 20 (Hii itatolewa kwa wachezaji waliofanya vizuri katika ligi ya vijana ya timu za Ligi Kuu ya Vodacom.
    Tuzo hiyo ya Mchezaji Bora wa Ligi ya Vijana itajulikana kama Tuzo ya Ismail Khalfan ikiwa ni heshima ya kumbukumbu ya mchezaji Ismail Khalfan wa Mbao FC aliyefia uwanjani katika mashindano hayo yaliyofanyika mkoani Kagera.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefikiria kutoa tuzo hiyo kama njia mojawapo ya kuonesha kuthamini kipaji cha mchezaji huyi wakati wa uhai wake.
    Kutokana na mabadiliko hayo tuzo zitakazotolewa katika sherehe hizo pamoja na Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya VPL ambayo ndiyo tuzo kuu, pia ni Bingwa wa Ligi Kuu, Mshindi wa Pili, Mshindi wa Tatu, Mshindi wa Nne na  Mfungaji Bora.
    Nyingine ni Mchezaji Bora wa Ligi Kuu, Golikipa Bora, Kocha Bora, Mwamuzi Bora, Mchezaji Bora wa Heshima, Mchezaji Bia anayechipukia, Goli Bora la Msimu, Mchezaji Bora wa Kigeni, Mchezaji Bora wa Chini ya Umri wa Miaka 20 na Timu Yenye Nidhamu.
    Tuzo za Bingwa, mshindi wa pili, wa tatu na wa nne na Mfungaji Bora hizi zipo kulingana na msimamo wa ligi ulivyo.
    Hata hivyo Mfungaji Bora safari hii kuna wachezaji wawili wamefungana, hivyo kamati itapitia vigezo vilivyopo katika Kanuni za kumpata Mfungaji Bora w Ligi Kuu Tanzania Bara ili kupata mshindi ambaye atatangazwa siku hiyo ukumbini.
    Wafuatao wameteuliwa kuwania tuzo hizo kutokana na vigezo mbalimbali:
    Mchezaji Bora wa Ligi Kuu
    Aishi MANULA - Azam
    Simon MSUVA - Yanga
    Shiza KICHUYA - Simba
    Haruna NIYONZIMA - Yanga
    Mohammed HUSSEIN – Simba
    (Majina ya wanaowania tuzo hiyo yalitolewa Jumatano iliyopita na upigaji kura unaendelea ukiwahusisha Makocha wa timu za Ligi Kuu na Makocha Wasaidizi,Wahariri wa habari za michezo na Manahodha wa timu za Ligi Kuu, ambapo mwisho wa kufanya hivyo ni Jumanne Mei 23 mwaka huu).
    KIPA BORA
    Aishi MANULA - Azam
    Owen CHAIMA - Mbeya City
    Juma KASEJA - Kagera Sugar
    KOCHA BORA
    Joseph OMOG - Simba
    Mecky MEXIME - Kagera Sugar
    Ettiene NDAYIRAGIJE - Mbao
    MWAMUZI BORA
    Shomari LAWI – Kigoma
    Elly SASII – Dar es Salaam
    Hance MABENA - Tanga
    MCHEZAJI BORA WA KIGENI
    Haruna NIYONZIMA - Yanga
    Method MWANJALE - Simba
    Yusuph NDIKUMANA - Mbao
    MCHEZAJI BORA ANAYECHIPUKIA
    Mbaraka ABEID - Kagera Sugar
    Shaaban IDD - Azam
    Mohammed ISSA - Mtibwa
    TUZO YA ISMAIL KHALFAN – (U-20)
    Shaaban IDD - Azam
    Abdalah MASOUD - Azam
    Mosses KITAMBI - Simba
    TUZO YA HESHIMA
    (Atatangazwa aliyeteuliwa siku hiyohiyo ya sherehe za tuzo).
    GOLI BORA LA MSIMU
    (Tayari yamepatikana mabao bora 10 ambayo yataoneshwa siku hiyo ukumbini ikiwemo lile bora la msimu mzima).
    TIMU YENYE NIDHAMU
    (Mshindi atatangazwa ukumbini siku hiyo kulingana na vigezo vilivyopo).
    WACHEZAJI 11 BORA WA MSIMU – VPL XI 2016/17
    (Watatangazwa ukumbini siku hiyo ya sherehe).
    Kamati inayohusika na usimamizi wa tuzo inawaomba wadau wote ambao wameombwa kupiga kura katika Tuzo ya Mchezaji Bora wafanye hivyo kulingana na fomu walizotumiwa na mchango wao una thamani kubwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NIYONZIMA, MWANJALI KUCHUANA NA NDIKUMANA MCHEZAJI BORA WA KIGENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top