• HABARI MPYA

  Tuesday, October 04, 2016

  TFF: MAREFA SIYO KOMPYUTA WASIKOSEE

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa amesema kwamba marefa ni binaadamu, si kompyuta hivyo si ajabu kukosea.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRU SPORTS – ONLINE jana kuhusu refa Martin Saanya ambaye anadaiwa kuvuruga mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya watani wa jadi, Simba na Yanga, Mwesigwa alisema kwamba wakati mwingine marefa wanasakamwa bure.
  “Kazi ya urefa ni ngumu, tunapowajadili tuwajadili kitaalamu.
  Huyu si kompyuta; Refa Martin Saanya anadaiwa kuvuruga mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya watani wa jadi, Simba na Yanga Jumamosi

  Hakuna binadamu aliyekamilika asilimia 100, hata kwenye maamuzi, si kwamba nawatetea, lazima tujue hii ni soka inayoendeshwa na binadamu, haiendeshwi na kompyuta,”alisema.
  Katibu huyo wa TFF alisema kwamba mara nyingi malalamiko dhidi ya marefa hutokea kwa upande unaopoteza mchezo, lakini timu ikishinda hailalamikii marefa. “Sisi hatutakiwi kuwa waamuzi wa waamuzi, tuache Kamati husika zichukue hatua,”alisema.
  Hata hivyo, kuhusu matatizo ya waamuzi, Mwesigwa alisema kwamba TFF sasa imeanza utaratibu wa kutayarisha marefa kuanzia umri mdogo katika vituo vya Jeshi vya Lugalo na Twalipo. 
  “Hata mechi ya Burnley na Arsenal (Ligi Kuu ya England juzi) refa alikosea pia. Hivyo si hapa kwetu tu, hata Ulaya na popote duniani, waamuzi ni binadamu wanakosea. Ila, TFF na Kamati ya Waamuzi tunajitahidi kuwanoa na mabadiliko tunayaona,”alisema.
  Kuhusu Sanya kulalamikiwa na Simba kuruhusu bao la mkono la Yanga na kukataa bao lao halali lililofungwa na Ibrahim Hajib, Mwesigwa amesema kwamba hawajapata barua rasmi ya malalamiko kutoka klabu hiyo hivyo hawezi kuzungumzia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF: MAREFA SIYO KOMPYUTA WASIKOSEE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top