• HABARI MPYA

  Monday, October 03, 2016

  AZAM YAMUUZA KLABU NYINGINE KIPRE TCHETCHE, TFF YAMUIDHINISHA KUCHEZA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imemuuza mshambuliaji wake, Kipre Herman Tchetche kwa klabu ya Al Suwaiq FC ya Ligi Kuu ya Oman kwa dola za Kimarekani 50, 000 zaidi ya Sh. Milioni 100 za Tanzania.
  Hatua hiyo imemfanya Tchetche, raia wa Ivory Coast aondoke klabu ya Al-Nahda Al-Buraimi pia ya Ligi Kuu ya Oman, ambayo ndiyo ilimtoa Azam FC akiwa amebakiza Mkataba wa mwaka mmoja.
  Licha ya Al Nahda kumalizana na Kipre Tchetche, lakini kwa kushindwa kulipa dola 50,000 za kuvunja Mkataba wa mchezaji huyo na Azam FC imemkosa.
  Kipre Tchetche sasa ni mchezaji wa klabu ya Al Suwaiq na Al Nahda tena 

  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kutoka Oman, Kipre alisema kwamba amejiunga na Suwaiq ambayo imelipa fedha za kuvunja Mkataba wa Azam FC na tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa Hati yake ya Uhamisho wake wa Kimataifa (ITC).
  Na amesema tayari amepata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC), ambayo sasa inamfanya aanze kucheza Ligi ya Oman.
  “Kwa sasa nipo klabu ya Suwaiq FC, baada ya Al Nahda kushindwa kulipa fedha za Azam,”amesema.
  Amesema haikuwa ngumu kwake kuhamia klabu nyingine, kwa kuwa hakuwa amechukua fedha za Al Nahda za usajili.
  “Mkataba ulikuwa haujakamilika, kwa sababu hawakuilipa Azam, hivyo klabu nyingine imelipa ada ya uhamisho na nimejiunga nayo, Taratibu za hapa, unaposaini hawakulipi hadi wapate ITC yako,”amesema.
  Awali, Tchetche alilazimika kurejea kwao, Ivory Coast mwezi uliopita baada ya Azam FC kugoma kumruhusu kujiunga na Al Nahda bila dola za Kimarekani 50,000.
  Na Azam ilifanya hivyo kwa sababu Tchetche aliondoka Dar es Salaam akiwa amebakiza Mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuichezea klabu hiyo tangu mwaka 2010.  
  Tchetche alirejea Oman wiki iliyopita kupigania uhamisho wake kutoka Azam FC, lakini baada ya Nahda kushindwa kumlipia ada ya uhamisho, Al Suwaiq imemchukua kufuatia kumalizana na timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake.   
  Kipre Tchetche alijiunga na Azam FC mwaka 2011 kwa pamoja na pacha wake, Kipre Michael Balou baada ya wote kung’ara katika kikosi cha Ivory Coast kilichokuja kucheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Challenge) Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM YAMUUZA KLABU NYINGINE KIPRE TCHETCHE, TFF YAMUIDHINISHA KUCHEZA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top