• HABARI MPYA

  Thursday, October 20, 2016

  SIMBA RAHA TUPU, MBAO WALIBANA WAKAACHIA WENYEWE, WAMEKUFA 1-0

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  BAO la dakika za lala salama la kiungp Muzamil Yassin limeifanya Simba SC iendelee kupaa kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbao FC ya Mwanza jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam
  Simba SC inafikisha pointi 26 baada ya kucheza 10 ikishinda nane na kutoa sare mbili – hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi sita zaidi.
  Mchezo huo uliochezeshwa na Hance Mabena, aliyesaidiwa na Hajji Mwalukuta wote wa Tanga na Michael Mkongwa wa Njombe, ulianza kwa kasi Simba washambulia zaidi lango la Mbao na dakika ya 18, shuti la Mrundi Laudit Mavugo lilipanguliwa na kipa Emmanuel Mseja na kumkuta Ibrahim Hajibu ambaye naye alipga nje.   
  Muzamil Yassin, mfungaji wa bao pekee la Simba dakika ya 87 katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbao FC ya Mwanza jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
  Mshambuliaji Mrundi wa Simba, Laudit Mavugo akiminyana na beki wa Mbao FC, Asante Kwasi raia wa Ghana

  Winga wa Simba, Shizza Kichuya akimtoka beki wa Mbao FC, Steve Mganya 

  Mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Hajib akipambana katikati ya wachezaji wa Mbao FC 

  Kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto akipambana na beki wa Mghana wa Mbao, Asante Kwasi    Mavugo tena dakika ya 20 akamdakisha kipa kwa shuti dhaifu baada ya krosi ya beki Mkongo, Janvier Besala Bokungu.  
  Mbao nao wakajibu shambulizi baada ya nyota wa zamani wa Yanga, Hussein Swedi kupiga shuti lililopanguliwa na kipa Muivory Coast, Vincent Angban dakika ya 30. Hajib akapiga nje tena dakika ya 41 na Mavugo akapiga juu ya lango dakika ya 43 wote wakiwa wamebaki na kipa wa Mbao.
  Pius Buswita alijichanganya dakika ya 48 na kushindwa kufunga akiwa kwenye nafasi nzuri ndani ya eneo la hatari la Simba.
  Kiungo mkongwe, Mwinyi Kazimoto akapiga nje dakika ya 54 na dakika ya 60 Blagnon akaifungia Simba bao lililokataliwa na refa Mabena kutoka Tanga akidai kwamba mchezaji aliunawa mpira kabla ya kufunga.
  Hatimaye Muzamil Yassin aliyesajiliwa msimu huu kutoka Mtibwa Sugar akawainua vitini mashabiki wa Simba dakika ya 87 akifunga bao zuri kwa kumalizia krosi ya mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Frederick Blagnon.
  Kwa ujumla Simba ilicheza vizuri tangu kipindi cha kwanza na kupeleka mashabulizi mengi langoni mwa Mbao, lakini bahati haikuwa yao ingawa pia leo winga Shizza Kichuya aliwekewa ulinzi mkali.
  Washambuliaji Ibrahim Hajib na Laudit Mavugo walioanzishwa pamoja leo hawakuweza kufurukuta mbele ya ukuta wa Mbao FC ulioongozwa na kiungo mkabaji kutoka Burundi, Youssuf Ndikumana.
  Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Hussein Sued aliishia kuwasumbua kidogo mabeki wa Simba, Mzimbabwe Method Mwanjali na Mganda, Juuko Murshid lakini hakuweza kufunga.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Method Mwanjali, Shizza Kichuya, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo/Frederick Blagnon dk51, Ibrahim Hajib/Mohamed Ibrahim dk58 na Mwinyi Kazimoto.
  Mbao FC; Emmanuel Mseja, Hussein Sued/Frank Damas dk64, Steve Mganya, Steve Kigocha, Asante Kwasi, Pius Buswita/Boniphace Maganga dk52, Youssouf Ndikumana, Robert Magadula, Salmin Hoza, Emmanuel Mvurekure na Dickson Ambundo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA RAHA TUPU, MBAO WALIBANA WAKAACHIA WENYEWE, WAMEKUFA 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top