• HABARI MPYA

  Monday, October 03, 2016

  SIMBA NA YANGA WAKETI FARAGHA NA SERIKALI KUHUSU VURUGU UWANJA WA TAIFA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  WIZARA ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo imekutana na viongozi wa klabu za Simba na Yanga pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo kujadili namna ya kudhibiti vurugu wakati mechi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Hatua hiyo inakuja kufuatia mashabiki wa Simba kufanya vurugu Uwanja wa Taifa Jumamosi baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
  Tambwe alifunga bao hilo dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
  Mashabiki wa Simba wakikimbia mabomu ya machozi wakati wa vurugu Uwanja wa Taifa, Jumamosi
  Eneo ambalo viti viling'olewa kwa wingi Uwanja wa Taifa, Jumamosi

  Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga. Na katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
  Kwa hali hiyo, mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani. Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo, Kaimu Mkurugenzi wa Michezo, Alex Nkenyenge amesema kwamba walikutana kufanya tathmini na kupenaa mikakati namna ya kudhibiti vurugu wakati wa mechi. 
  Alipoulizwa kwamba kikao ni ishara ya klabu kuruhusiwa kuendelea kuutumia Uwanja huo, kufuatia tamko la kuzuiliwa jana, Nkenyenge alisema; “Hatukujadili kuruhusiwa kuutumia Uwanja. Na kufungiwa kwao ni maamuzi ya Waziri, 
  Tumepeana mikakati tu kwa faida ya baadaye,”aamesema.
  Zaidi ya viti 1781 vilivunjwa Jumamosi na mashabiki wa Simba kutokana na vurugu hizo – wakati pia kabla ya mchezo, mashabiki wa timu zote mbili walivunja mageti mawili makubwa katika kulazimisha kuingia kinyume cha utaratibu.
  Kiasi cha kati ya Sh. Milioni 350 na 400 zilikusanywa katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 1-1, ambao mashabiki waliingia kwa tiketi za Elektroniki.
  Na jana, Serikali ilitoa tamko la kuzuia mapato ya mchezo huo hadi hapo itakapokata gharama za uharibifu uliosababishwa na vurugu hizo sambamba na kutangaza kuzizuia kuutumia Uwanja huo hadi hapo itakapoamua vinginevyo.
  Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye alisema jana kwamba Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya kihuni vya namna hiyo na wanachukua hali kali ili liwe fundisho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA NA YANGA WAKETI FARAGHA NA SERIKALI KUHUSU VURUGU UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top