• HABARI MPYA

    Monday, October 03, 2016

    OMOG AMSTAHI REFA SAANYA, AAMUA KWENDA KUIONGEZEA MAKALI SIMBA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mcameroon wa Simba SC, Joseph Marius Omog amekataa kumzungumzia refa Martin Saanya, lakini amesema anakwenda kuwanoa zaidi vijana wake, ili waendeleze rekodi ya kutofungwa katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Simba SC juzi ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na mahasimu wake wa jadi, Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Na akizungumza jana mjini Dar es Salaam, Omog alisema kwamba baada ya matokeo hayo wanarudi kambini kujiandaa na michezo ijayo. “Tunakwenda kuendelea kujituma na mazoezi, ili tuwe katika ubora wetu na kuendeleza rekodi yetu nzuri katika Ligi Kuu,”alisema kocha huyo wa zamani wa Azam FC.
    Akiuzungumzia mchezo wa juzi, Omog alisema ulikuwa mkali ambao ulikutanisha timu mbili kubwa zenye wachezaji wakiubwa pia. “Tulikuwa pale kwa ajili ya kushinda, lakini malengo hayakutimia,”alisema Omog aliyewahi kufundisha AC Leopard ya Kongo Brazzaville na kuipa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2012.
    Hata hivyo, kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon, alikataa kulizungumzia bao la Yanga lililotaka kuvuruga amani Uwanja wa Taifa juzi – na kwa ujumla hakutaka kumjadili refa, akisemaa; “Sina maelezo” baada ya kutakiwa kuzungumzia uchezeshaji wa refa na bao la wapinzani wake.
    “Hatukushinda kwa sababu tulikutana na timu bora yenye uzoefu mzuri,”alisema Omog ambaye Azam FC watamkumbuka kwa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2013/2014.
    Mechi ya juzi iliingiwa doa baada ya mashabiki wa Simba kufanya vurugu Uwanja wa Taifa kufuatia Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, AmissiTambwe.
    Tambwe alifunga bao lake dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
    Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.
    Katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele. Na mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani.
    Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OMOG AMSTAHI REFA SAANYA, AAMUA KWENDA KUIONGEZEA MAKALI SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top