• HABARI MPYA

    Sunday, June 12, 2016

    PLUIJM AMUACHA JUMA ABDUL SAFARI YA UTURUKI, BOSSOU NAYE HAENDI KAMBINI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mholanzi wa Yanga, Hans van der Pluijm hajamchukua beki wa kulia, Juma Abdul katika kikosi cha wachezaji 21 wanaosafiri kwenda Uturuki kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mouloudia Olympique Bejaia Juni 19, mwaka huu.
    Mchezo huo wa Kundi A utafanyika Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria na Yanga itawasili nchini humo siku mbili kabla ya mechi.
    Abdul aliumia kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) Mei 25 mwaka huu Yanga ikishinda 3-1 na akaenda kujitonesha akiichezea timu ya taifa, Taifa Stars ikifungwa 2-0 na Misri Juni 4, mwaka huu.
    Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm usiku huu akiwa na Msaidizi wake, Juma Mwambusi wakati wa safari ya Uturuki

    Na kwa sababu hiyo, Juma Abdul anatakiwa kuwa nje kwa wiki mbili, hivyo beki mpya, Hassan Kessy anaweza kuanza mapema kuteleza upande wa kulia baada ya kusajiliwa mwezi uliopita kutoka kwa mahasimu, Simba SC.
    Kikosi cha Yanga hivi sasa kipo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa safari ya Alfajiri ya kwenda Uturuki na mbali na Juma Abdul, wengine wanaoachwa ni Vincent Bossou, ambaye hajarejea kutoka kwao Ivory Coast na majeruhi Malimi Busungu, kipa Benedictor Tinocco na mshambuliaji Paul Nonga ambao hawamo kwenye programu ya kocha, wakati kinda Yussuf Mhilu hatakwenda kwa sababu jina lake halijasajiliwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
    Bossou ataungana na timu Algeria baada ya kumaliza matatizo yake ya kifamilia maana yake hata kambi ya Uturuki hataiwahi.
    Kiungo Deus Kaseke (kushoto) na mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma wakati wa safari usiku huu JNIA

    Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ anasafiri lakini hatacheza mechi hiyo ya kwanza ya Kundi A kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi nyekundu, aliyopewa kwenye mchezo uliopita dhidi ya Sagrada Esperanca nchini Angola. 
    Kiungo Salum Telela ni mchezaji pekee aliyemaliza msimu na Yanga ambaye hatasafiri, kwa sababu hajapewa Mkataba mpya baada ya kumaliza wa awali.
    Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Morocco, Bouchaib El Ahrach atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Redouane Achik na Youssef Mabrouk.
    Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28 katika mchezo wake wa pili wa Kundi A.
    Na katika mchezo huo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa kutoka nchi tatu tofauti, ambao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O'michael wa Eritrea.
    Timu nyingine katika Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu, mchezo ambao utachezeshwa na marefa wa Shelisheli Bernard Camille, Hensley Danny Petrousse na Eldrick Adelaide.
    Juma Abdul (kushoto) akiichezea Yanga dhidi ya Al Ahly Aprili 9, mwaka huu katika Ligi ya Mabingwa Afrika

    Kikosi kamili cha Yanga kinachokwenda Uturuki ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya.
    Mabeki; Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.
    Viungo; Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Godfrey Mwashiuya.
    Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony na Amissi Tambwe.
    Msafara umeongozwa na Kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa Mohammed Mpogolo na Meneja Hafidh Saleh. Safari njema Yanga. Kila la heri.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PLUIJM AMUACHA JUMA ABDUL SAFARI YA UTURUKI, BOSSOU NAYE HAENDI KAMBINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top