• HABARI MPYA

  Saturday, June 04, 2016

  MUHAMAAD ALI AFARIKI DUNIA AKIWA ANA UMRI WA MIAKA 74

  BONDIA bora zaidi kuwahi kutokea duniani, Muhammad Ali amefariki dunia akiwa ana umri wa miaka 74 baada ya miaka 32 ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kupooza na kutetemeka (Parkinson). 
  Fundi huyo wa mchezo wa ngumi, amefariki dunia jana akiwa amezungukwa na familia yake, siku moja baada ya kukimbizwa hospitali baada ya kuzidiwa na kushindwa kupumua vizuri. 
  "Baada ya miaka 32 ya kusumbuliwa na ugonjwa wa Parkinson, Muhammad Ali amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 74. Bingwa mara tatu wa dunia amefariki jioni hii,"amesema Msemaji wa Ali.


  Bondia shujaa: Ali akitembea kibabe ulingoni baada ya kumuangusha bondia mkali, George Foreman raundi ya nane katika pambano lililopewa jina Rumble in the Jungle mjini Kinshasa, Zaire (sasa DRC) mwaka 1974  PICHA ZAIDI GONGA HAPA

  Familia ya Ali imesema mazishi yake yatafanyika nyumbani kwake Louisville, Kentucky, na kushukuru umma kwa ushirikiano wao. 
  Ali alikuwa akipatiwa tiba katika hospitali Phoenix, Arizona, baada ya hali yake kuwa mbaya Alhamisi na alikimbizwa hospitali akiwa 'hajitambui'. 
  Jina lake la kuzaliwa ni Cassius Clay na alizaliwa Louisville, Kentucky Januari 17, mwaka 1942. 
  Mabondia wenzake kama Sugar Ray Leonard, MIke Tyson wametoa heshima zao za mwisho kwa marehemu Ali: "Maombi na baraka kwa shujaa wangu, rafiki yangu na bila shaka bingwa wa wakati wote@MuhammadAli!"
  Mara ya mwisho Ali kuonekana hadharani ilikuwa Aprili katika tamasha la "Celebrity Fight Night" mjini Arizona. 
  Ali aligundulika kuwa na ugonjwa wa Parkinson miaka mitatu baada ya kustaafu ndondi mwaka 1981 akiwa na rekodi ya kushinda mapambano 56 na kushindwa matano.
  Ali aliingia kwenye mgogoro na serikali ya Marekani kwa zaidi ya miaka mitatu miaka ya 1960 wakati alipokataa kujiunga na jeshi la nchi hiyo kwa ajili ya vita ya Vietnam na akashitakiwa na kutiwa hatiani.
  Mahakama ya juu kabisa ya Marekani ikaipundua hukumu hiyo na kauchiwa kabla ya kwenda kushinda mataji mawili ya dunia ya uzito wa juu kisha kustaafu mwaka 1981. Pumzika kwa amani fundi Ali. Dunia itakukumbuka daima.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MUHAMAAD ALI AFARIKI DUNIA AKIWA ANA UMRI WA MIAKA 74 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top