• HABARI MPYA

  Thursday, August 08, 2019

  MALINDI YAICHOMOLEA YANGA SC DAKIKA YA MWISHO ZANZIBAR, SARE 1-1 AMAAN

  Na Asha Kigundula, ZANZIBAR
  TIMU Yanga SC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Malindi SC katika mchezo wa kirafiki usiku wa leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Winga Deus Kaseke alitangulia kuifungia Yanga SC bao dakika ya 16 kabla ya kiungo mshambuliaji Mohammed Ahmed Adam kuisawazishia Malindi SC dakika ya 90.
  Ushindi huo unakuja siku moja baada ya Yanga kushinda 4-1 dhidi ya Mlandege SC usiku wa jana katika mechi nyingine ya kujipima nguvu kujiandaa na msimu mpya.
  Mabao ya Yanga SC jana yalifungwa na nyota wa kigeni, Mnyarwanda Patrick Sibomana dakika ya 26, Mganda Juma Balinya dakika ya 36, Mnamibia Sadney Urikhob dakika ya 42 na mzalendo Mrisho Ngassa dakika ya 65.

  Bao pekee na la kufutia machozi la Mlandege SC lilifungwa na Hassan Ramadhani dakika ya 88 na Yanga SC itaondoka kesho kurejea Dar es Salaam, tayari kwa mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana Jumamosi Uwanja wa Taifa.
  Katika mechi zake za awali za kujiandaa na msimu mpya, Yanga SC ilitoa sare ya 1-1 na Kariobangi Sharks ya Kenya Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, ilishinda 2-0 dhidi ya Friends Rangers jana, 7-0 dhidi ya ATN, 2-0 dhidi ya Moro Kids na 1-0 dhidi ya Mawenzi Market zote mjini Morogoro.
  Yanga SC na Township Rollers zitarudiana Agosti 25 mjini Gaborone na mshindi wa jumla atakutana na mshindi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Metacha Mnata/Ramadhani Kabwili dk46, Cleophas Sospeter, Gustafa Simon, Moustafa Suleiman/Ally Ally dk46, Said Juma ‘Makapu’, Abdulaziz Makame/Feisal Salum dk46, Deus Kaseke, Raphael Daudi, David Molinga ‘Falcao’/Jaffar Mohamed dk65, Maybin Kalengo/Issa Bigirimana dk46 na Mrisho Ngassa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MALINDI YAICHOMOLEA YANGA SC DAKIKA YA MWISHO ZANZIBAR, SARE 1-1 AMAAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top