• HABARI MPYA

    Sunday, August 11, 2019

    GENK YA SAMATTA YAANZA KUPUNGUA UTAMU, YACHAPWA MECHI YA PILI MFULULIZO YA LIGI

    Na Mwandishi Wetu, GENK
    MABINGWA watetezi, KRC Genk jana wamepoteza mechi ya pili mfululizo ya Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji baada ya kuchapwa 2-0 nyumbani na Zulte-Waregem Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
    Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na mfungaji bora wa timu msimu uliopita, Mbwana Samatta alicheza kwa dakika zote 90 jana lakini kwa mara nyingine akashindwa kufunga.
    Mabao yaliyoizamisha Genk jana yalifungwa na washambuliaji Mnorway, Henrik Rorvik Bjordal dakika ya sita na Mrundi, Saido Berahino dakika ya 78.

    Mbwana Samatta akimtoka beki wa Zulte-Waregem usiku wa jana Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk

    Mechi ya kwanza ya Ligi, Genk ilichapwa 3-1 na wenyeji, KV Mechelen Agoti 3 Uwanja wa AFAS- Achter de Kazerne mjini Mechelen, Malines siku ambayo Samatta alifunga bao lake la kwanza la msimu dakika ya dakika ya 45 na ushei akimalizia pasi ya kiungo Mbelgiji, Bryan Heynen. 
    Na hilo lilikuwa bao la kusawazisha baada ya KV Mechelen kutangulia kwa bao la Muivory Coast, William Togui dakika ya 18, kabla ya washambuliaji wenzake, Msweden Gustav Engvall kufunga la pili dakika ya 77 na Mbrazil, Igor Alberto de Camargo kufunga la tatu dakika ya 80.
    Samatta mwenye umri wa miaka 26 jana, ameichezea mechi ya 159 KRC Genk katika mashindano yote akiwa amefunga mabao 63 tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 125 na kufunga mabao 48, kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, katika Super Cup mechi moja na Europa League mechi 24 katika mabao 14.
    Kikosi cha KRC Genk jana kilikuwa: Coucke, Uronen, Lucumi, Dewaest, Maehle, Berge/Piotrowski dk89, Heynen, Hagi/Odey dk68, Paintsil/Benson dk81, Ito na Samatta
    Setup Zulte-Waregem: Bossut, De fauw, Zarandia, Larin, Govea, Bjordal, Seck, Bürki, Humphreys, Berahino na Deschacht.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: GENK YA SAMATTA YAANZA KUPUNGUA UTAMU, YACHAPWA MECHI YA PILI MFULULIZO YA LIGI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top