• HABARI MPYA

    Wednesday, April 03, 2019

    BOCCO MCHEZAJI BORA, AUSSEMS KOCHA BORA LIGI KUU MWEZI MACHI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    NAHODHA wa  Simba SC ya Dar es Salaam, John Raphael Bocco amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Machi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.
    Bocco ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Donald Ngoma wa Azam FC na Jaffari Kibaya wa Mtibwa Sugar SC alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
    Kwa mwezi huo wa Machi, Simba ilicheza mechi tatu na kushinda zote na mshambuliaji huyo, Bocco alitoa mchango mkubwa kwa timu yake akifunga mabao manne na kuifanya Simba iendelee kubaki nafasi ya tatu.

    Kwa upande wa Ngoma alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Azam FC kwa mwezi huo, ambapo timu yake ilicheza mechi tatu ikishinda zote na kuendelea kubaki nafasi ya pili, akifunga mabao manne.
    Mshambuliaji Kibaya alikuwa chachu ya mafanikio ya Mtibwa Sugar SC ambayo ilicheza mechi nne, ikishinda tatu na kupoteza moja, huku ikipaa kutoka nafasi ya 12 hadi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 20.
    Kwa kuibuka mchezaji bora, Bocco atazawadiwa sh. 1,000,000 (milioni moja) na kombe (trophy) kutoka kwa wadhamini wa tuzo Biko Sports pamoja na kisimbusi kutoka Azam TV ambao ndiyo wenye haki ya matangazo ya TPL.
    Pia Kamati ya Tuzo, imemchagua Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems kuwa Kocha Bora wa Machi akiwashinda Kocha Mkuu wa Azam, Abdul Mingange na Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila.
    Aussems ameifanya Simba iendelee kung’ara katika ligi hiyo ambapo kwa mwezi huo ilishinda michezo yote mitatu iliyocheza ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo.
    Kocha huyo pia atazawadiwa sh. 1,000,000 (milioni moja) na kombe (trophy) kutoka Biko Sports.
    TFF ina utaratibu wa kuwazadiwa wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BOCCO MCHEZAJI BORA, AUSSEMS KOCHA BORA LIGI KUU MWEZI MACHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top