• HABARI MPYA

  Saturday, December 15, 2018

  ‘KAPTENI’ BOCCO AFUNGA BAO MUHIMU LA UGENINI KWA PENALTI SIMBA SC YACHAPWA 2-1 NA NKANA FC KITWE

  Na Mwandishi Wetu, KITWE
  SIMBA SC imepoteza mchezo wa kwanza wa hatu ya mwisho ya mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa 2-1 na wenyeji, Nkana FC Uwanja wa Nkana mjini Kitwe, Zambia.
  Sasa Wekundu wa Msimbazi, Simba SC watahitaji ushindi wa 1-0 kwenye mchezo wa marudiano Desemba 23 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam ili kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo, ambayo mara ya kwanza na ya mwisho walifika mwaka 2003.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Salisu Basheer aliyesaidiwa na washika vibendera Peter Eigege Ogwu na Efosa Celestine Igudia wote wa Nigeria, hadi mapumziko Nkana FC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  John Bocco ameifungia Simba leo kwa penalti baada ya Meddie kagere kuangushwa
  Shiza Kichuya aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Emmanuel Okwi leo

  Emmanuel Okwi akipambana na mchezaji wa Nkana FC leo Uwanja wa Nkana mjini Kitwe 

  Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji Ronald Kampamba kwa shuti kali dakika ya 27 akimalizia pasi ya beki Muivory Coast, Ben Bahn Adama.
  Na kipindi cha pili Nkana FC walikianza vizuri na kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Simba SC hadi kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 56 kupitia kwa Kelvin Kampamba.
  Kocha Mbelgiji wa Simba SC, Patrick J Aussems alifanya mabadiliko baada ya bao hilo akimtoa mshambuliaji Emmanuel Okwi na kumuingiza kiungo Shiza Kichuya.
  Mabadiliko hayo yaliisaidia Simba SC kupata bao la ugenini, lililofungwa na Nahodha John Raphael Bocco kwa penalti dakika ya 74 baada ya mshambuliaji Myarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere kuangushwa kwenye boksi.
  Kikosi cha Nkana FC kilikuwa; Allan Chibwe, Hassan Kessy, Ben Banh, Musa Mayeko, Harrison Chisala, Ronald Kampamba/Festus Mbewe dk84, Walter Bwalya, Kelvin Kampamba, Richard Ocran, Duncan Otieno na Shadrack Malambo/Freddy Tshimenga dk86.
  Simba SC; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, James Kotei, Clatous Chama, Emmanuel Okwi/Shiza Kichuya dk60, John Bocco/Hassan Dilunga dk90+2 na Meddie Kagere.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ‘KAPTENI’ BOCCO AFUNGA BAO MUHIMU LA UGENINI KWA PENALTI SIMBA SC YACHAPWA 2-1 NA NKANA FC KITWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top