• HABARI MPYA

    Tuesday, December 25, 2018

    THOMAS ULIMWENGU ASAINI MIAKA MIWILI KUJIUNGA NA JS SAOURA YA ALGERIA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Klabu ya Js Saoura (JSS) ya Algeria iliyofuzu kucheza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Ulimwengu amesaini mkataba huo leo, ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu avunje mkataba na klabu ya El Hilal ya Sudan aliyoichezea kwa miezi mitano tu baada ya kujiunga nayo akitokea AFC Eskilstuna ya Sweden.
    Ulimwengu alijiunga na Hilal baada ya kuwa nje kwa muda mrefu sababu ya maumivu ya goti ambayo yalimfikisha katika hospitali ya Taasisi ya Sayansi ya Michezo mjini Cape Town, Afrika Kusini kwa upasuaji mwaka jana na kupitia kipindi kirefu cha mazoezi ya kujiweka fiti.

    Thomas Ulimwengu akiwa ameshika jezi ya JS Saouara baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili leo

    Maumivu hayo yalimzuia kuichezea klabu ya Eskilstuna aliyojiunga nayo Januari mwaka jana akitokea Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kuvunja mkataba. 
    Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi mwaka 2011  alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
    Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
    Ulimwengu alihamia Ulaya baada ya kushinda mataji makubwa akiwa na  Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: THOMAS ULIMWENGU ASAINI MIAKA MIWILI KUJIUNGA NA JS SAOURA YA ALGERIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top