• HABARI MPYA

    Monday, December 31, 2018

    SIMBA SC YAPELEKA KIKOSI KAMILI MICHUANO YA KOMBE LA MAPINDUZI ZANZIBAR

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU bingwa ya soka Tanzania Bara, Simba SC itaondoka Jumatano ya Januari 2, mwakani kwenda Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, ikiwa na kikosi chake kamili.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara amewaambia Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam kwamba watakwenda na kikosi kamili ili kufanya vizuri kwenye mashindano hayo.
    Manara, mtoto wa mchezaji nyota wa zamani wa Yanga, Sunday Manara ‘Computer’ amesema pamoja na dhamira ya kufanya vizuri, lakini pia wanataka kutumia michuano hiyo kuipa mazoezi timu yao ambayo inajiaanda na mechi yake ya kwanza ya Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura ya Algeria.
    Amesema kwamba mechi dhidi ya timu hiyo mpya ya mshambuliaji Mtanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu itapigwa Jumamosi ya Januari 12, Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kuanzia Saa 10:00 jioni.
    Manara amesema kwamba kikosi cha kwanza kitarejea Dar es Salaam mapema hata Simba ikifuzu kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya JS Saoura na kikosi cha pili kitabaki Zanzibar kumalizia michuano hiyo.
    “Na kwa kuwa fainali ya Mapinduzi hufanyika Januari 13, iwapo Simba itafuzu basi kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya wachezaji kurejea visiwani Zanzibar kucheza fainali hiyo,”amesema Manara na kuongeza;
    “Ikumbukwe Simba inathamini sana Mapinduzi hayo matukufu na ndiyo maana tumeamua kupeleka kikosi kamili ili kuwapa burudani Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla, licha ya kukabiliwa na mechi ngumu ya kimashindano ya ligi ya Mabingwa barani Afrika,”.
    Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2019 imepangwa kuanza kesho, Januari 1 hadi 13, mwakani ikifanyika katika miji ya Pemba na Unguja ikishirikisha timu tisa.
    Hizo ni KVZ, KMKM, Jamhuri, Chipukizi, Mlandege na Malindi kutoka Zanzibar na Azam, Simba na Yanga za Tanzania Bara.
    Kundi A linajumisha timu za Chipukizi, Mlandege, KMKM na Simba wakati Kundi B litakuwa na timu za KVZ, Malindi, Jamhuri, Azam na Yanga na kama ilivyo kawaida, mechi zote za mashindano hayo zitaonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam kupitia chaneli zake mbalimbali.
    Bingwa wa Mapinduzi 2019 atajipatia kitita cha Sh. Milioni 15, ambazo ni ongezeko la Sh. Milioni 5 kutoka zawadi za mwaka huu, Mshindi wa pili atapata Sh. Milioni 10 badala ya Milioni 5 za msimu uliopita.
    Mechi zote za mashidano hayo msimu huu zitafanywa Uwanja wa Amaan uliopo Unguja hadi Nusu Fainali wakati mchezo wa Fainali utafanyika Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba.
    Mechi za Amaan zitakuwa zinachezwa kuanzia Saa 10:15 jioni na Saa 2:15 usiku huku mechi ya fainali ikitarajiwa kuchezwa kuanzia Saa 9:30 Alasiri.
    Simba SC itafungua dimba na Chipukizi Januari 4, kabla ya kumenyana na KMKM na kumalizia na Mlandege Januari 8, mechi zote zikanzia Saa 2:15 usiku.
    Ikumbukwe Simba pia imepangwa Kundi D pamoja na JS Saoura ya Algeria, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Kundi A limezikutanisha timu za na Lobi Stars ya Nigeria, Wydad Casablanca ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
    Kundi B linaungwa na FC Platinums ya Zimbabwe, Horoya A.C ya Guinea, Esperance ya Tunisia na Orlando Pirates ya Afrika Kusini, wakati Kundi C limezikutanisha Ismailia FC ya Misri, CS Constantine ya Algeria, Club Africain ya Tunisia na TP Mazembe ya DRC.
    Mechi za hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa zitaanza Januari 11 mwakani na kufikia tamati Machi 17. Droo ya Robo Fainali itafanyika Machi 23, 2019.
    Simba SC wataanzia nyumbani Januari 11 dhidi ya J.S. Saoura kabla ya kusafiri kuwafuata AS Vita Januari 18 mjini Kinshasa na Al Ahly Februari 1 mjini Cairo kukamilisha mechi za mzunguko wa kwanza.
    Mzunguko wa pili itaanzia nyumbani Februari 12 dhidi yq Al Ahly mjini Dar es Salaam, kabla ya kusafiri kuwafuata J.S. Saoura nchini Algeria Machi 8 na kurejea nyumbani kumalizia na AS Vita Machi 15.
    Simba imefuzu tena kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 15, kufuatia mara ya mwisho kufika hatua hiyo mwaka 2003 ikiitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
    Na msimu huu wamefuzu kwa kuitoa Nkana FC ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-3, wakishinda 3-1 nyumbani baada ya kufungwa 2-1 ugenini.    
    Wakati mwaka 2003 ilifuzu ikiwa chini ya kocha Mkenya, James Aggrey Siang’a kipa wa zamani wa Harambee Stars, sasa marehemu, safari hii Simba SC imefuzu ikiwa chini ya kocha Mbelgiji, Patrick J. Aussems mwenye umri wa miaka 53, beki wa zamani wa Ubelgiji aliyechezea klabu za RCS Visé, Standard Liege, K.A.A. Gent, R.F.C. Seraing na ES Troyes AC.
    Na kabla ya Simba, Aussems amefundisha klabu za ES Troyes AC, SS Saint-Louisienne, Capricorne Saint-Pierre, Stade Beaucairois, Stade de Reims, KSA ya Cameroon, SCO Angers, Evian Thonon Gaillard F.C., Shenzhen Ruby, Chengdu Blades, AC Leopards ya Kongo na timu ya taifa ya Nepal.  
    Rekodi nzuri ya Simba SC Klabu Bingwa Afrika ni kufika Nusu Fainali mwaka 1974 ikiitoa Hearts Of Oak ya Ghana kabla ya kutolewa na Mehalla El Kubra ya Misri, lakini matokeo yake mazuri zaidi kwenye michuano ya Afrika ni kufika fainali ya iliyokuwa michuano ya Kombe la CAF mwaka 1993 na kufungwa na Stella Club Adjame, maarufu Stella Abidjan.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAPELEKA KIKOSI KAMILI MICHUANO YA KOMBE LA MAPINDUZI ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top