• HABARI MPYA

    Thursday, December 20, 2018

    YANGA SC YAICHAPA AFRICAN LYON 1-0 NA KUZIDI KUPAA KILELENI LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imezidi kupepea kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushinid wa bao 1-0 dhidi ya African Lyon jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
    Ushindi huo uliotokana na bao pekee la beki Abdallah Hajji Shaibu ‘Ninja’ kipindi cha pili, unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 47 baada ya kucheza mechi 17, sasa ikiizidi kwa pointi saba, Azam FC iliyo nafasi ya pili kwa pointi zake 40 za mechi 16, wakati mabingwa watetezi, Simba SC ni wa tatu kwa pointi zao 30 za mechi 13.    
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Erick Onoka aliyesaidiwa na Gasper Ketto na Abdallah Uhako, Yanga ilipata pigo kipindi cha kwanza baada ya wachezaji wake wawili kuumia na kutoka.


    Alianza kiungo Jaffar Mohammed ambaye alimpisha Deus Kaseke dakika ya 17 akafuatia kipa Ramadhani Kabwili ambaye nafasi yake ilichukuliwa Klaus Kindoki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dakika ya 40.
    Yanga hawakuwa katika ubora wao wa siku za karibuni na haikuwa ajabu kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza bila kupata bao pamoja na kutengeneza nafasi mbili nzuri.
    Kipindi cha pili Yanga SC walirudi na kasi ya kushambulia kutafuta mabao, lakini kitu kimoja kiliwachelewesha kutokuwa na ushirikiano katika safu ya ushambuliaji.
    Mara kadhaa mkongwe wa Burundi, Amissi Joselyn Tambwe alilazimisha kupiga kujaribu kufunga badala ya kumpasia mshambuliaji mwenzake, Mkongo Hertier Makambo aliyekuwa kwenye nafasi nzuri.
    Hata hivyo, beki Abdallah Hajji Shaibu ‘Ninja’ aliwainua majukwaani mashabiki wa Yanga baada ya kufunga kwa kichwa dakika ya 64 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo Ibrahim Ajibu Migomba.
    Katika kuhakikisha timu inapata bao, Tambwe aliusindikiza nyavuni kwa kichwa pia mpira huo wakati unavuka mstari wa goli, lakini hapana shaka lilikuwa bao la beki Mzanzibar, Abdallah Shaibu ‘Ninja’. 
    Kikosi cha African Lyon kilikuwa; Douglas Kasebo, Daudi Salim, Kassim Simbaulanga, Emmanuel Simwanza, Roland Msonjo, Jabir Aziz, Khalfan Mbarouk, Said Mtikila, Kassim Mdoe, Hamisi Thabit/Hamisi Balozi dk75 na Baraka Jaffar.
    Yanga SC; Ramadhani Kabwili/Klaus Kindoki dk40, Paul Godfrey, Gardiel Michael, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Kelvin Yondan, Maka Edward, Ibrahim Ajibu, Pius Buswita, Heritier Makambo, Amissi Tambwe na Jaffar Mohammed/Deus Kaseke dk17.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAICHAPA AFRICAN LYON 1-0 NA KUZIDI KUPAA KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top